Baba bosi, Neymar nahodha Santos
Muktasari:
- Katika maboresho ya uongozi yaliyofanyika baba wa mchezaji huyo, Neymar Santos Sr amepata nafasi ya juu katika uongozi wa klabu hiyo, akilamba ukurugenzi mtendaji, huku mwanawe akiiongoza timu ndani ya uwanja akiwa nahodha.
SAO PAOLO, BRAZIL: FAMILIA ya mwanasoka nyota, Neymar da Silva Santos Junior imeshika hatamu za uongozi wa Klabu ya Santos ya Brazil.
Mshambuliaji wa zamani wa Barcelona ya Hispania, PSG ya Ufaransa na Al Hilal ya Saudi Arabia kwa sasa ndiye nahodha wa kikosi hicho ambacho kilimtangaza katika maisha ya soka duniani kabla ya kuzurura timu mbalimbali kisha kurejea kukichezea.
Katika maboresho ya uongozi yaliyofanyika baba wa mchezaji huyo, Neymar Santos Sr amepata nafasi ya juu katika uongozi wa klabu hiyo, akilamba ukurugenzi mtendaji, huku mwanawe akiiongoza timu ndani ya uwanja akiwa nahodha.
Klabu hiyo yenye historia kubwa nchini Brazil imethibitisha uongozi mpya jambo linalotarajiwa kuzua mjadala ikizingatiwa kwamba kwa sasa kikosi hicho hakifanyi vizuri katika mashindano mbalimbali kinayoshiriki. Nafasi aliyokabidhiwa baba’ke Neymar ilikuwa wazi kwa mwaka mmoja na nusu, na ataitumikia angalau hadi mwishoni mwa mwaka huu. Nchini Brazil, mzazi huyo wa staa wa kizazi hiki Barazil anafahamika zaidi kwa jina la utani la Neymar Pai ambaye alikuwa wakala wa wachezaji akiwamo mwanaye.
Neymar Jr alirejea katika klabu yake ya utotoni, Santos, 2025 ambapo urejeo wake ulikuwa wa hisia kubwa kwa mashabiki. Hata hivyo, uteuzi wa baba yake katika nafasi ya uongozi sasa umegeuza kurejea kwa nyota huyo kuwa mradi mkubwa wa kifamilia ndani ya klabu hiyo. Hivyo, mmoja wa kina Neymar atakuwa akisimamia maamuzi ya kiutawala, huku mwingine akiwaongoza wachezaji ndani ya uwanja.
Santos, inayofahamika pia kwa jina la utani la El Peixe, inashika nafasi ya tisa katika Ligi Kuu Brazil (Serie A), ikiwa imebakiza mechi nne kabla ya msimu kumalizika. Hali hiyo inakuja baada ya klabu hiyo kunusurika kushuka daraja kwa tofauti ndogo msimu uliopita.
Hali ya mambo imekuwa ngumu zaidi kutokana na kukosekana kwa nyota wao namba 10, ambapo adhabu ya kufungiwa imemfanya Neymar kukosa mechi mbili za mwisho za Santos, jambo linaloongeza presha kwa timu hiyo katika hatua muhimu ya kumaliza msimu.
Kati ya matarajio makubwa ya uongozi mpya, hasira za mara kwa mara za mashabiki na kurejea kwa nahodha wao, Santos sasa imeweka sehemu kubwa ya mustakabali wake mikononi mwa familia ya Neymar.
Je, uamuzi huo utazaa matunda na kuirejesha Santos katika mafanikio, au utaongeza zaidi mijadala na mabishano kuliko utukufu wa klabu hiyo?