Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Grealish aomba radhi, aanza upya Everton

GREALISH Pict

Muktasari:

  • Everton iliibuka na ushindi wa mabao 4-1 katika mchezo huo, ambao ulikuwa sehemu ya hatua za kumrejesha kiungo huyo katika mazingira ya kikosi chini ya kocha David Moyes.

LIVERPOOL, ENGLAND: KIUNGO mshambuliaji wa Everton, Jack Grealish, ameanza ukurasa mpya ndani ya kikosi hicho baada ya kurejea uwanjani na kuomba radhi kwa mashabiki kufuatia sakata la utovu wa nidhamu lililomuweka nje ya kikosi.

Grealish, mwenye umri wa miaka 31, alicheza kwa mara ya kwanza tangu kusimamishwa kutokana na kukosa mazoezi, akishiriki mchezo wa kirafiki wa faragha dhidi ya Derby County uliofanyika kwenye Uwanja wa Hill Dickinson.

Everton iliibuka na ushindi wa mabao 4-1 katika mchezo huo, ambao ulikuwa sehemu ya hatua za kumrejesha kiungo huyo katika mazingira ya kikosi chini ya kocha David Moyes.

GREA 01

Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Grealish alitumia nafasi hiyo kuomba radhi kwa mashabiki na wote wanaohusika na klabu hiyo.

Alisema amefurahi kurejea mazoezini na kucheza pamoja na wenzake baada ya kupitia siku kadhaa za mazoezi maalumu.

Pia aliomba radhi kwa mashabiki kwa kushindwa kuisaidia timu katika michezo ya hivi karibuni.

Grealish alisema anaipenda Everton na anatamani kurejea haraka kucheza mbele ya mashabiki wa timu hiyo akiwa amevaa jezi ya bluu.

GREA 02

Nyota huyo aliingia kwenye mgogoro baada ya kukosa safari ya Everton kwenda kucheza dhidi ya Arsenal, akieleza kuwa alikuwa mgonjwa.

Hata hivyo, klabu ilithibitisha kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu za nidhamu, jambo lililomfanya Moyes kumuweka nje ya kikosi kwa michezo miwili dhidi ya Newcastle United na Coventry City.

Kurejea kwake katika mchezo dhidi ya Derby kulikuwa mara ya kwanza kuvaa jezi ya Everton tangu walipofungwa mabao 2-0 na Chelsea Oktoba 17.

GREA 03

Katika mchezo huo wa kirafiki, Charly Alcaraz alifunga mabao mawili, huku Jonathan Nsangou mwenye umri wa miaka 16 na Christian Norgaard wakifunga bao moja kila mmoja. Derby walipata bao lao kupitia Lars-Jørgen Salvesen.

Mchezo huo pia uliwapa nafasi ya kupata muda wa kucheza wachezaji wengine akiwemo Tyler Dibling, Hayden Hackney, Merlin Rohl, Michael Keane, Ainsley Maitland-Niles na kipa Tom King.

Awali, Moyes alikuwa amekuwa mwangalifu kuzungumzia suala la Grealish, akisema mchezaji huyo hakuwa tayari kurejea kikosini na kwamba klabu ingefanya uamuzi pale hali yake itakapokuwa sawa.

Hata hivyo, kocha huyo alidokeza kuwa milango haijafungwa kwa kiungo huyo kurejea kwenye kikosi cha kwanza.

Grealish alijiunga na Everton kwa mkopo akitokea Manchester City baada ya kushindwa kupata nafasi ya kudumu katika kikosi cha mabingwa hao wa England.

GREA 04

Mchezaji huyo aliyeigharimu City Pauni milioni 100 mwaka 2021 alikuwa sehemu muhimu ya kikosi kilichotwaa mataji matatu msimu wa 2022/23.

Alikuwa amecheza michezo sita pekee katika kipindi chake cha pili cha mkopo Everton kabla ya kukumbwa na sakata hilo la nidhamu.

Msimu uliopita alicheza michezo 22 na kufunga mabao mawili, lakini safari yake ilikatishwa na majeraha.

Mkataba wake na Manchester City unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

Sasa, baada ya kuomba radhi na kurejea uwanjani, Grealish anahitaji kuthibitisha kwa vitendo kwamba amejifunza kutokana na makosa yake na yuko tayari kupigania nafasi yake Everton.