Huyu Gallagher? Spurs watampenda tu
Muktasari:
- Hayo ni maoni ya Gus Poyet, ambaye pia aliwahi kucheza kiungo kwa wapinzani hao wakubwa mwanzoni mwa miaka ya 2000.
LONDON, ENGLAND: MASHABIKI wa Tottenham Hotspur wameelezwa kwamba watampenda mara moja kiungo mchapakazi Conor Gallagher bila kujali historia yake Chelsea.
Hayo ni maoni ya Gus Poyet, ambaye pia aliwahi kucheza kiungo kwa wapinzani hao wakubwa mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Mruguay huyo anaamini kuwa nyota huyo wa zamani wa Chelsea ambaye alihamia Spurs kutoka Atletico Madrid wiki hii, atawashawishi haraka mashabiki wote waliokuwa na mashaka kutokana na mtindo wake wa kujituma na kujitoa uwanjani.
Nguvu na bidii ya mchezaji huyo mpya wa Pauni 35 milioni pia inaweza kusaidia Spurs kushinda mechi zake katika kuweka hai msimu wao.
Alipoulizwa ni kwa kiasi gani ni vigumu kushinda mioyo ya mashabiki wa Spurs ukiwa mchezaji wa zamani wa Chelsea, Poyet aliambia SunSport kupitia Stake Casino: “Kwa Conor, hili si tatizo kabisa.
“Ni rahisi kwake kwa sababu ya jinsi anavyocheza soka. Analeta nguvu na msukumo uwanjani, na hicho ndicho mashabiki wa Spurs wanataka.
“Wanataka kuona kujitoa, wachezaji wanaopigania nembo ya klabu, na hilo ndilo Conor analeta.
“Anakimbia, anafanya kazi kwa bidii, analeta shauku na anaweza kuonyesha hilo mara moja na kuwavuta mashabiki upande wake.
“Ni usajili wa hali ya juu sana kwa Spurs.
“Anatoa kila kitu uwanjani, anachukua jukumu, na hicho ndicho Spurs wanahitaji kwa sasa.
“Usajili huu unaweza kuwasaidia Spurs kwa kiasi kikubwa, na mtindo wake wa kucheza unaweza pia kuwahamasisha wachezaji wengine kufikia kiwango chake.”
Tottenham ilichukua hatua haraka kumsajili Gallagher, Jumatano iliyopita baada ya Rodrigo Bentancur, kufanyiwa upasuaji wa jeraha kubwa la misuli ya paja.
Gallagher anatoka katika familia ya mashabiki wa Chelsea na alicheza mechi 95 Stamford Bridge kabla ya kuuzwa Atletico Madrid miezi 18 iliyopita. Poyet alihama moja kwa moja Chelsea kwenda Spurs 2001 kwa ada ya Pauni 2.2 milioni.