He! Eti Ugarte ana gundu
Muktasari:
- Man United ilichapwa 2-1 uwanjani Villa Park, hivyo kushuka zaidi katika mbio za kufukuzia ubingwa wa Ligi Kuu England.
MANCHESTER, ENGLAND: KIUNGO wa Manchester United, Manuel Ugarte amedaiwa kwamba ndiye gundu kubwa kwenye kikosi hicho wakati inachapwa na Aston Villa uwanjani Villa Park, Jumapili iliyopita.
Man United ilichapwa 2-1 uwanjani Villa Park, hivyo kushuka zaidi katika mbio za kufukuzia ubingwa wa Ligi Kuu England.
Licha ya kucheza vizuri sehemu kubwa ya mchezo huo na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga, kikosi hicho cha kocha Ruben Amorim kilimalizwa na mchezaji mmoja tu, Morgan Rogers, aliyefunga mara mbili huku Man United ikipata bao la kujipoza kupitia kwa Mbrazili, Matheus Cunha.
Lakini, matokeo hayo yamemponza mchezaji mmoja na kutolewa mbuzi wa kafara kwamba ndiye chanzo cha timu kupoteza.
Shabiki mmoja aliandika kwenye X: “Ugarte ana gundu.”
Mwingine amesema: “Gundu la Ugarte limeendelea tena.”
Shabiki wa tatu amesema: “Gundu la Ugarte limeendelea ni mechi saba sasa alizoanza timu imepoteza.”
Na takwimu zinawatisha zaidi mashabiki wa Man United, ambapo katika mechi tisa ambazo Ugarte ameanza, hakuna ushindi, sare moja na vichapo vinane.
Hiyo ni rekodi ya ajabu sana kwa mchezaji mmoja wa Man United kwenye michuano baada ya Kleberson kuwahi kufanya hivyo kati ya Januari 2004 na Mei 2005. Hata hivyo, Mbrazili huyo rekodi zake ni nzuri kuliko za Ugarte, ambapo katika mechi 10, alitoka sare saba na vichapo vitatu.
Ugarte alipata nafasi ya kuanza Villa Park kutokana na Casemiro kutumikia adhabu ya kadi na Kobbie Mainoo kuwa majeruhi.