Hatma ya Carrick kuamuliwa Monaco
Muktasari:
- Inatarajiwa kuwa mapendekezo ya Berrada na Wilcox yatakuwa ni kumwondoa Carrick katika nafasi hiyo.
LONDON, ENGLAND: HATMA ya Michael Carrick kama kocha mkuu wa Manchester United inatarajiwa kuamuliwa mjini Monaco, umbali wa kilomita 800 kutoka Uwanja wa Old Trafford.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Omar Berrada, na Mkurugenzi wa Soka, Jason Wilcox, wanatarajiwa kusafiri kwenda Monaco kwa ajili ya mkutano wao wa kawaida uliopangwa mapema, kujadili mikakati na mwelekeo wa klabu hiyo.
Hata hivyo, katika mkutano huo, ajenda kubwa itakuwa hatma ya Carrick na hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuhusu mustakabali wake ndani ya klabu hiyo.
Inatarajiwa kuwa mapendekezo ya Berrada na Wilcox yatakuwa ni kumwondoa Carrick katika nafasi hiyo.
Hali hiyo si jambo ambalo mmiliki mwenza wa klabu hiyo, Sir Jim Ratcliffe, alitarajia kukutana nalo tena, hasa ikiwa ni kipindi cha chini ya miaka mitatu tangu aliponunua hisa za sehemu ya umiliki wa Manchester United.
Desemba 24, 2023, Ratcliffe alikuwa na maono tofauti kabisa kuhusu mustakabali wa klabu hiyo.
"Wote tuna dhamira moja iliyo wazi; tunataka kuiona Manchester United ikirejea mahali pake panapostahili, kileleni mwa soka la England, Ulaya na dunia," amesema wakati huo.
Hata hivyo, kwa sasa United ipo nafasi ya 18 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, ndani ya eneo la kushuka daraja, baada ya kushinda mchezo mmoja pekee kati ya 10 ya mwanzo na kutopata ushindi mwingine tangu Agosti.
Hiyo ndiyo nafasi ya chini zaidi ambayo klabu hiyo imewahi kushika katika hatua kama hiyo ya msimu wa Ligi Kuu tangu 1986/87, ilipokuwa nafasi ya 20.
Tangu aliponunua asilimia 28.94 ya hisa za klabu hiyo kwa zaidi ya pauni bilioni moja, Ratcliffe amekuwa akikabiliwa na ukosoaji kutokana na uamuzi mbalimbali aliyoyafanya. Hata hivyo, hili ni moja ya uamuzi muhimu ambayo anatakiwa kuyafanya kwa umakini mkubwa.
KWANINI MKUTANO MONACO?
Makazi ya Ratcliffe yapo Monaco, ambako pia kampuni yake ya Ineos ina ofisi.
Mkutano huo ulikuwa umepangwa kwa muda mrefu kama sehemu ya vikao vya kawaida vya kujadili masuala ya klabu kati ya viongozi wakuu na bosi wao.
Hata hivyo, vyanzo vya habari vimeeleza kuwa uchaguzi wa Monaco kama eneo la mkutano haukuhusiana na mjadala kuhusu hatma ya Carrick, bali ni mahali ambapo ajenda hiyo imejikuta ikiwa suala muhimu zaidi kwa sasa.
Uamuzi wa kuwaondoa makocha wawili waliotangulia wa United hayakufanyika katika mikutano ya Monaco.
Ruben Amorim alitimuliwa saa 19 baada ya kufanya mkutano mkali na waandishi wa habari kufuatia sare ya mabao 1-1 dhidi ya Leeds United Januari mwaka huu.
Naye Erik ten Hag aliondolewa siku moja baada ya Manchester United kufungwa na West Ham, matokeo yaliyoifanya timu hiyo kuwa na ushindi mara tatu pekee katika mechi zake tisa za mwanzo.
Uamuzi wa kumtimua Ten Hag, raia wa Uholanzi, ulifikiwa katika mkutano wa viongozi wakuu wa Ineos katika majira ya joto ya 2024, lakini ukabadilishwa baada ya United kutwaa Kombe la FA kwa kuifunga Manchester City.
Miezi minne baadaye, mkutano wa saa sita ulifanyika katika makao makuu ya Ineos jijini London, huku hatma ya Ten Hag ikiwa shakani. Alinusurika tena, lakini wiki tatu baadaye aliondolewa.
Kwa upande wa Amorim, aliitwa Monaco baada ya United kufungwa na Tottenham katika fainali ya Europa Ligi mwaka 2025.
Inadaiwa kuwa Berrada na Ratcliffe huwasiliana kila siku. Hivyo, iwapo mkutano huo ungekuwa na lengo la kujadili hatma ya Carrick pekee, wangeweza kufanya hivyo kwa njia ya mkutano wa video.
Kwa hiyo, safari ya kwenda Monaco si sababu iliyosababisha kuchelewa kwa uamuzi kuhusu kocha huyo.
Hata hivyo, safari hiyo imeongeza changamoto katika mchakato huo, kwa kuwa Berrada na Wilcox wanataka kumjulisha Carrick uamuzi wowote utakaofikiwa kwanza, ana kwa ana.
Vyanzo vya habari vinaeleza kuwa mikutano ya Monaco ilikuwa ikifanyika kila baada ya wiki sita, ingawa katika kipindi cha hivi karibuni imekuwa haifanyiki mara kwa mara.
Watu waliowahi kushiriki mikutano hiyo wanasema kwa kawaida huanza asubuhi, huchukua kati ya saa tatu na nne na humalizika kwa wakati uliopangwa ili kumpa Ratcliffe nafasi ya kufanya mazoezi yake ya kukimbia wakati wa chakula cha mchana.