Harry Kane: England hii? Tunabeba
Muktasari:
- England ya Kocha Thomas Tuchel ilihitimisha mechi zake za kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 kibabe kabisa ilipopata ushindi wa tisa mfululizo, shukrani kwa mabao mawili yaliyofungwa na straika Kane kwenye mechi dhidi ya Albania.
LONDON, ENGLAND: STRAIKA Harry Kane amesifu kikosi cha sasa cha England kina wachezaji wenye viwango bora kabisa kuwahi kucheza nao katika maisha yake ya soka.
England ya Kocha Thomas Tuchel ilihitimisha mechi zake za kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 kibabe kabisa ilipopata ushindi wa tisa mfululizo, shukrani kwa mabao mawili yaliyofungwa na straika Kane kwenye mechi dhidi ya Albania.
Sasa, Kane, ambaye ni nahodha wa kikosi hicho cha Three Lions, amefikisha mabao 78 kwenye soka la kimataifa, ikiwa ni bao moja zaidi ya aliyofunga gwiji wa soka wa Brazil, Pele.
Mabao hayo mawili ya Kane yalitengenezwa na wachezaji waliotokea benchini Bukayo Saka na Marcus Rashford hiyo ni kuonyesha upana wa kikosi hicho cha kocha Tuchel kitakachokwenda kwenye fainali hizo za Amerika Kaskazini.
Kane, 32, amesema: “Ni nzuri kama ambavyo tumekuwa siku zote. Ukitazama kikosi cha wachezaji 11 walioanza na wale wanaoingia kutokea benchini, tutakwenda kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia tukiwa moja ya timu zinazopewa nafasi kubwa.”
Rekodi ya Tuchel ya ushindi wa asilimia 100 kwenye mechi za kufuzu zimeishuhudia England kuzoa pointi 24 kati ya 24 Kundi K, ikifunga mabao 22 bila ya kuruhusu bao lolote.
Kane alifunga bao lake la kwanza kwenye dakika 74 baada ya kumalizia kona ya Saka kabla ya kufunga kwa kichwa akiunganisha krosi safi ya Rashford dakika nane baadaye.
Kocha Tuchel, ambaye alifanya mabadiliko ya wachezaji saba katika mechi hiyo ya Albania, amepongeza kasi ya kufunga mabao ya straika huyo wa Bayern Munich, Kane.