Haaland azua hofu Man City
Muktasari:
- Haaland, mwenye umri wa miaka 26, alitolewa dakika ya 67 katika mchezo huo wa Ligi ya Mataifa ya Ulaya uliochezwa Porto, Ureno, baada ya kuonyesha benchi kuwa ana maumivu.
LONDON, ENGLAND: MSHAMBULIAJI Erling Haaland amewaacha Manchester City na presha baada ya kuomba kutolewa katika mchezo wa Norway dhidi ya Ureno, huku hali yake ikiwa haijafahamika baada ya kuonekana akichechemea.
Haaland, mwenye umri wa miaka 26, alitolewa dakika ya 67 katika mchezo huo wa Ligi ya Mataifa ya Ulaya uliochezwa Porto, Ureno, baada ya kuonyesha benchi kuwa ana maumivu.
Wakati akitoka uwanjani, Norway ilikuwa sare ya bao 1-1 na Ureno, baada ya Kristoffer Ajer kuipatia Norway bao la kuongoza kabla ya Joao Cancelo kusawazisha.
Dakika 12 baada ya Haaland kutolewa, Goncalo Ramos aliifungia Ureno bao la pili na kuipa ushindi wa mabao 2-1.
Hali hiyo imeongeza hofu Manchester City, hasa kutokana na umuhimu wa Haaland katika kikosi hicho. Mshambuliaji huyo amefunga mabao matano katika mechi tano za Ligi Kuu England msimu huu.
Haaland si mchezaji pekee wa City aliyepata changamoto ya majeraha akiwa kwenye majukumu ya timu ya taifa wakati huu.
Kiungo Nico O'Reilly alirejea Manchester baada ya kupata tatizo la kiafya akiwa na timu ya taifa ya England, huku Rico Lewis akipandishwa kutoka kikosi cha England chini ya miaka 21 kuchukua nafasi yake.
City inatarajiwa kurejea uwanjani mwishoni mwa wiki hii dhidi ya liverpool baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa, huku ikisubiri taarifa zaidi kuhusu hali ya Haaland.
Hofu hiyo imekuja wakati City ikiwa pia inakabiliwa na changamoto ya kesi yake ya ukiukaji wa kanuni za kifedha za Ligi Kuu England, ambapo klabu hiyo imekutwa na hatia ya sehemu kubwa ya mashtaka 115 iliyokuwa ikikabiliwa nayo. City imeendelea kupinga makosa hayo na imekata rufaa dhidi ya uamuzi huo.