Viktor Gyokeres apeleka kicheko Emirates Stadium
Muktasari:
- Straika mpya wa Emirates, Gyokeres alitarajia kuongoza safu ya ushambuliaji ya miamba hiyo kwenye mchezo wa usiku wa Jumatano dhidi ya Villarreal kwenye uwanja wa nyumbani huko London. Macho ya wengi yalikuwa kwa Gyokeres, atakuwa amefanya nini kumaliza kiu ya mashabiki.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL inaamini kwamba hatimaye imempata straika wa ndoto yao kwa ajili ya kuongoza safu yao ya ushambuliaji kwa miaka kadhaa mbele baada ya kumsajili mkali wa kimataifa wa Sweden, Viktor Gyokeres kwenye dirisha hili.
Straika mpya wa Emirates, Gyokeres alitarajia kuongoza safu ya ushambuliaji ya miamba hiyo kwenye mchezo wa usiku wa Jumatano dhidi ya Villarreal kwenye uwanja wa nyumbani huko London. Macho ya wengi yalikuwa kwa Gyokeres, atakuwa amefanya nini kumaliza kiu ya mashabiki.
Kikosi kile cha Arsenal kilichocheza bila ya kupoteza mechi chini ya Arsene Wenger kilikuwa na mastaa kama Thierry Henry na Dennis Bergkamp kwenye fowadi yao. Tangu hapo, Arsenal imekuwa ikitafuta straika mwingine wa mabao, Namba 9, ambaye hasumbuliwi sana na majeraha baada ya kufanya usajili wa wakali kibao ambao wameshindwa kabisa kuonyesha makali ya kutosha.
Hii hapa orodha ya mastraika matata waliowahi kunaswa na Arsenal wakati wanatafuta staa wa kuja kuwapigia mabao ya uhakika kama kipindi cha kina Henry na Bergkamp.
1. Robin van Persie; Mwaka 2004, ikiwa bado kwenye makali ya kucheza msimu wote bila ya kupoteza mechi kwenye ligi, Arsenal ilimsajili straika Mdachi, Van Persie kutoka Feyenoord kwa ada ya Pauni 2.75 milioni. Wastani wake wa kufunga ulikuwa mzuri sana, lakini shida alisumbuliwa sana na majeraha kabla ya kutimkia Manchester United alikoenda kubeba taji la ligi.
2. Nicklas Bendtner; Katika kuelekea msimu wao wa mwisho kwenye Uwanja wao wa zamani wa Highbury mwaka 2005, Arsenal ilimsajili straika Bendtner wakati huo akiwa na miaka 17 na kuwa kwenye kikosi hicho kwa miaka tisa. Bendtner hakuwa na kiwango cha kutosha na aliishia tu kutolewa kwa mikopo kadhaa kabla ya kuondoka jumla.
3. Emmanuel Adebayor; Alifunga mabao 12 katika msimu wake wa kwanza uwanjani Emirates baada ya kutua Arsenal akitokea Monaco mwaka 2006. Staa huyo wa Togo, Adebayor angeweza kufanikiwa zaidi, lakini aliondoka kwenda Manchester City na baadaye Tottenham na kuwakasirisha Arsenal.
4. Eduardo; Straika aliyekuwa na kipaji matata cha kufunga mabao, lakini majeraha yalimtibulia maisha. Eduardo alitua Arsenal akitokea Dinamo Zagreb mwaka 2007 na alikuwa vizuri hadi hapo alipovunjika mguu dhidi ya Birmingham.
5. Marouane Chamakh; Fowadi huyo wa Morocco alitua Arsenal akitokea Bordeaux mwaka 2010, lakini kinachokumbukwa kuhusu yeye ni staili ya nywele zake. Alikuwa anachelewa sana na hilo ndilo lililokuwa tatizo lake kubwa.
6.Park Chu-Young; Hii ni kali. Staa huyo wa Monaco alikuwa akifanya vipimo vya afya huko Lille wakati alipopata taarifa kwamba Arsenal inamtaka. Aliwasili London ndani ya saa 24 kwenda kukamilisha dili hilo la kutua Emirates.
7. Lukas Podolski; Moja ya usajili matata kabisa kuwahi kufanyika kwenye kikosi hicho na alikuwa kipenzi cha mashabiki, lakini Podolski hakufikia kabisa kwenye viwango vilivyokuwa vimetarajiwa. Alitua akitokea Cologne na baadaye alitibuana na kocha Wenger jambo lililomfanya atolewe kwa mkopo Inter Milan.
8. Olivier Giroud; Katika kipindi hicho cha Podolski, Giroud naye alisajiliwa baada ya kuipa Montpellier taji la Ligue 1. Mabao 105 katika misimu sita, straika huyo Mfaransa alikuwa na kitu cha kuonekana, lakini alikuwa akipoteza nafasi nyingi.
9. Yaya Sanogo; Staa huyo wa zamani wa Auxerre alikuwa kwenye kikosi cha Arsenal kwa miaka minne, lakini alianzishwa mara mbili tu kwenye Ligi Kuu England. Hilo linaonyesha Sanogo alikwenda Arsenal kujaza wingi wa watu tu.
10. Danny Welbeck; Alikuwa kwenye viwanja vya mazoezi vya Arsenal akiwa na timu ya taifa ya England wakati anakamilisha uhamisho wake kutoka Man United. Bahati mbaya kwa Welbeck, maisha yake ya Arsenal yalitibuliwa na majeraha makubwa ya goti na enka.
11. Lucas Perez; Staa huyo Mhispaniola alinaswa kwa ada ya Pauni 17 milioni kutokea Deportivo La Coruna. Alifunga hat-trick kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Basel, lakini baada ya hapo, Perez alishindwa kuonyesha makali, akianzishwa mara mbili tu kwenye mechi za Ligi Kuu England.
12. Alexandre Lacazette; Huu ulikuwa usajili wa mwisho wa kocha Wenger, ambapo Arsenal ililipa Pauni 52 milioni kumsajili. Staa huyo alikuwa na wastani mzuri wa kufunga mabao hasa katika mechi ambazo Arsenal ilihitaji ushindi.
13. Pierre-Emerick Aubameyang; Staa huyo wa Gabon anakumbukwa kwa kufunga mara mbili kwenye fainali ya Kombe la FA dhidi ya Chelsea mwaka 2020. Lakini, mambo yake ya nje ya uwanja yalimfanya atibuane na kocha Arteta.
14. Gabriel Jesus; Alijiunga Arsenal mwaka 2022 kwa ada ya Pauni 45 milioni akitokea Man City, lakini idadi ya mabao ya staa huyo wa Kibrazili bado si tamu sana katika kikosi cha Emirates na ndiyo maana ameletwa straika mpya. Majeraha yamemuathiri sana.
15.Kai Havertz; Staa mwingine wa kutoka Chelsea, ambapo Arsenal ililipa Pauni 65 milioni kunasa saini yake. Mjerumani huyo bado ana uwezo wa kuonyesha makali yake Emirates licha ya ujio wa straika mpya, Gyokeres.
16. Eddie Nketiah; Mashabiki wa Arsenal walikuwa na matumaini makubwa kwamba straika aliyekulia kwenye akademia yao atapata mafanikio makubwa. Alikuwa na nafasi kubwa, lakini aliuzwa kwenda Crystal Palace mwaka 2024.