Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aibu utaona wewe! Carrick akomaa kusaka ushindi

CARRICK Pict

Muktasari:

  • United ina pointi saba baada ya mechi tisa. Ikiendelea kwa kiwango hicho hadi mwisho wa msimu, haitafikisha pointi 30. Hata hivyo, historia inaonyesha kuwa kushuka daraja kwa klabu hiyo bado ni jambo lisilo la kawaida.

LONDON, ENGLAND: MANCHESTER United imejikuta katika nafasi ya 17 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kufungwa mabao 2-0 na Chelsea Jumamosi. Kocha Michael Carrick amesema timu inapaswa kuendelea kupambana na kushinda mechi, huku hali yake ya sasa ikizua maswali kuhusu uwezekano wa kushuka daraja.

“Tunapaswa kuendelea kusonga mbele na kushinda michezo, ndivyo ilivyo,” amesema Carrick.

Kocha huyo aliwahi kushuka daraja akiwa West Ham mwanzoni mwa maisha yake ya soka. Msimu wa 2002/03, West Ham ilikuwa na kikosi kilichoonekana kuwa na uwezo wa kubaki Ligi Kuu, kikijumuisha kipa wa England, David James, pamoja na Carrick, Joe Cole, Jermain Defoe na Trevor Sinclair, ambao kila mmoja alicheza zaidi ya mechi 40 katika mashindano yote.

Hata hivyo, West Ham ilimaliza nafasi ya tatu kutoka mwisho ikiwa na pointi 42. Hadi sasa, hiyo ndiyo idadi kubwa zaidi ya pointi ambayo timu imeshuka nayo daraja katika msimu wa Ligi Kuu wenye mechi 38.

United ina pointi saba baada ya mechi tisa. Ikiendelea kwa kiwango hicho hadi mwisho wa msimu, haitafikisha pointi 30. Hata hivyo, historia inaonyesha kuwa kushuka daraja kwa klabu hiyo bado ni jambo lisilo la kawaida.

United haijawahi kuwa ndani ya eneo la kushuka daraja baada ya kucheza mechi tisa au zaidi tangu Novemba 1986. Nafasi yake ya chini zaidi baada ya mechi tisa au zaidi tangu wakati huo ilikuwa ya 17 msimu wa 1989/90, nafasi ambayo imerudia sasa, kwa kiasi kikubwa kutokana na matokeo ya timu nyingine Jumamosi.

CARR 01

Klabu hiyo haijashinda mechi yoyote kati ya tisa zilizopita katika mashindano yote, rekodi yake mbaya zaidi tangu msimu wa 1988/89. Ushindi wake pekee wa Ligi Kuu msimu huu ulikuwa dhidi ya Ipswich mwezi Agosti, baada ya kutoka nyuma.

Mashabiki wa United wana kumbukumbu ya hivi karibuni ya kuiona timu yao katika sehemu za chini za msimamo. Msimu wa 2024/25, ilikuwa nafasi ya 16 chini ya Ruben Amorim baada ya mechi 37. Hata hivyo, ilikuwa na pengo la pointi 14 dhidi ya Leicester iliyokuwa nafasi ya tatu kutoka mwisho, na haikuwa katika hatari ya kushuka daraja wakati wowote.

Tottenham, kwa upande mwingine, ilikaribia zaidi kushuka daraja msimu uliopita. Ilikuwa nafasi ya tatu kutoka mwisho, ikiwa nyuma ya West Ham kwa pointi mbili zikiwa zimesalia mechi nne.

Kwa hivyo, kushuka daraja kunawezekana, ingawa bado ni vigumu kutarajia klabu inayotarajiwa kuingiza zaidi ya pauni700 milioni  msimu huu kumaliza katika nafasi tatu za mwisho.

CARR 02

Alipoulizwa kama wachezaji wake wanaweza kubadili mtazamo na kukabiliana na hali hiyo, Carrick amesema wanaweza kuangalia namna ya kupanda haraka kwenye msimamo kwa kushinda mechi.

“Unaweza kuitazama hivyo, au unaweza kuangalia jinsi unavyoweza kupanda haraka kwenye msimamo ukishinda mechi. Hivyo ndivyo tunavyopaswa kukabiliana nayo,” amesema.

United itahitaji kuanza kushinda ili kujiondoa kwenye hali hiyo. Mchezo wake unaofuata ni dhidi ya Aston Villa, utakaopigwa Old Trafford Novemba 8. Katika mechi saba zitakazofuata, pia itakutana na Liverpool, Newcastle na Arsenal ugenini.

Bado hakuna taarifa rasmi kuhusu mustakabali wa Carrick, ingawa kabla ya kipigo cha Jumamosi ilitarajiwa kuwa angeiongoza timu hiyo katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya AS Roma kesho Jumanne. Hata hivyo, hali ya sasa haijazoeleka kwa United, na wachezaji wengi wanahitaji kuongeza kiwango chao.

CARR 03

United haitakuwa na Lisandro Martinez katika mchezo dhidi ya Villa baada ya beki huyo kuonyeshwa kadi nyekundu dhidi ya Chelsea. Aliyekuwa mwamuzi wa fainali ya Kombe la Dunia, Darren Cann, alieleza tukio hilo kuwa “lisiloelezeka”.

Mustakabali wa Martinez wa muda mrefu ndani ya klabu haujulikani. Mkataba wake unaisha mwishoni mwa msimu, huku historia yake ya majeraha ikizua maswali kuhusu kama United inapaswa kutumia kipengele cha kuongeza mkataba kwa msimu mwingine. Hata hivyo, hawezi kuondoka kabla ya dirisha la usajili la Januari kufunguliwa.


CARR 02

ATHARI ZA KIFEDHA ZA KUSHUKA DARAJA

Baada ya mechi tisa pekee, bado ni mapema kutathmini kikamilifu athari za kifedha ambazo kushuka daraja kungeiletea United. Hata hivyo, makadirio yaliyotolewa Mei na mchambuzi wa fedha za soka Paul Quinn, anayejulikana kama The Esk, yalionyesha kuwa Tottenham ingeweza kupoteza mapato kati ya pauni milioni 197 hadi 235 endapo ingeshuka daraja.

United ni miongoni mwa klabu zinazopata mapato makubwa zaidi kutokana na haki za matangazo ya televisheni, hivyo malipo ya msaada kwa klabu zinazoshuka daraja yasingeweza kufidia pengo lake la mapato.

Haijulikani kama mikataba ya wachezaji wa United ina vipengele vinavyopunguza mishahara endapo timu itashuka daraja. Klabu hiyo pia ina mapato makubwa ya kibiashara, lakini haijabainika kwa kiwango gani mapato hayo yangeathiriwa.

United ina deni la pauni1.15 bilioni, linalojumuisha hati fungani zilizofanyiwa marekebisho Juni kwa riba kubwa zaidi, mkopo wa muda mfupi unaoweza kuongezwa na malipo ya ada za usajili ambazo bado hazijalipwa.

Klabu hiyo inatarajia pia kuanza mashauriano na mashabiki kuhusu uwanja mpya, kabla ya kuwasilisha mipango ya mwisho mwishoni mwa 2027 au mwanzoni mwa 2028. Katika kipigo dhidi ya Chelsea, mashabiki wa United walirudia kupinga mpango huo.