Doncic vs Wembanyamavita tuzo ya MVP 2026/27
Muktasari:
- Masupastaa Luka Doncic na Victor Wembanyama wameanza msimu kwa viwango vya kuvutia wakiwa na timu zao za Los Angeles Lakers na San Antonio Spurs mtawalia.
WASHINGTON, MAREKANI: MBIO za kuwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu (MVP) wa NBA kwa msimu wa 2026/27 bado zipo katika hatua za mwanzo, lakini wachezaji wawili tayari wameweka viwango vya juu vya kipekee.
Masupastaa Luka Doncic na Victor Wembanyama wameanza msimu kwa viwango vya kuvutia wakiwa na timu zao za Los Angeles Lakers na San Antonio Spurs mtawalia.
Takwimu zao zinaonyesha namna mbili tofauti za kutawala mchezo wa kikapu, lakini wote wameanza kutoa hoja nzito za kuwania tuzo hiyo kubwa zaidi ya mchezaji binafsi katika ligi hiyo.
Doncic anaonekana kuwa na dhamira ya kufanya kila mechi kuwa bonge la shoo la kuonyesha uwezo wake mkubwa wa kufunga, kwani katika mechi 12 alizocheza, nyota huyo wa Slovenia amekuwa akipata wastani wa pointi 39, ribaundi 7.2 na pasi za mwisho 7.8 kwa kila mchezo.
Kwa sasa anaongoza NBA kwa wastani wa ufungaji na anafurahia mwanzo bora zaidi wa mashambulizi katika maisha yake ya kikapu.
Kinachovutia zaidi ni kwamba kiwango chake cha uzalishaji wa pointi hakitokani tu na kufanya majaribio mengi ya kufunga, bali ana wastani wa asilimia 48.6 wa mafanikio ya mipira anayotupia kuelekea kapuni, asilimia 40.6 katika mipira ya pointi tatu na asilimia 86.5 mipira ya adhabu.
Akiwa na umri wa miaka 27, Doncic anaunganisha uzalishaji wa pointi binafsi na uwezo wa kuwashirikisha wachezaji wenzake katika mchezo.
Pia anarekodi wastani wa mipira 1.9 anayoiba kwa kila mchezo, ingawa wastani wake wa kupoteza mipira 4.8 unaonyesha ukubwa wa majukumu aliyonayo katika kuandaa mashambulizi ya Lakers. Iwapo ataendelea na kiwango hicho cha ufungaji, itakuwa vigumu kumuweka pembeni katika mjadala wa kuwania tuzo ya MVP.
WEMBANYAMA YUPO SANA
Upande mwingine wa mbio hizo kuna mchezaji anayeonekana kuvuka mipaka ya kawaida ya uwezo wa kimwili katika mchezo wa kikapu ambaye ni Victor Wembanyama aanayepata wastani wa pointi 28.6, ribaundi 11.6 na kuzuia mipira mitano (blocks) 4.3 katika mechi za mwanzo akiwa na San Antonio Spurs. Na cha kushangaza zaidi, anafikia takwimu hizo akiwa uwanjani kwa wastani wa dakika 29.8 pekee kwa kila mchezo.
Nyota huyo wa Ufaransa hahitaji kucheza kwa dakika nyingi ili kubadilisha matokeo ya mchezo, na uwezo wake wa kujilinda umekuwa wa kiwango cha juu akirekodi wastani wa kuzuia mipira 4.3 na kuiba mipira 1.1 kwa kila mchezo.
Pia amekuwa akifunga kwa mafanikio ya asilimia 53.5 ya mipira anayotupa kuelekea kapuni, jambo linaloonyesha uwezo wake wa kutumia vyema nafasi anazopata karibu na kapu pamoja na vipaji vyake vya kipekee vya kimwili.
Katika mchezo mmoja, Wembanyama alirekodi pointi 26, ribaundi 11, pasi sita za mwisho na kuzuia mipira mitano. Hiyo ilikuwa mechi nyingine aliyofanikiwa kufikisha takwimu za double-double, ambazo hutokea mchezaji anapofikisha idadi ya tarakimu mbili katika vipengele viwili tofauti.
Hoja za Wembanyama kuwania MVP hazijajengwa kwenye takwimu zake za ushambuliaji pekee, kwani uwepo wake eneo la chini ya kapu unaweza kuvuruga kabisa mipango ya wapinzani, kulinda kapu na kuipa San Antonio nafasi ya kufanya mashambulizi ya haraka baada ya kuzuia mipira ya wapinzani.
Iwapo ataendelea kucheza katika kiwango hicho, anaweza kujiweka katika kundi la wachezaji waliotawala NBA kwa kiwango cha juu zaidi katika historia ya hivi karibuni.
KILA MMOJA UFUNDI WAKE
Wachezaji hao wawili kila mmoja ana namna yake ya kutawala mchezo. Ulinganisho kati ya Doncic na Wembanyama unavutia kwa sababu wana mitindo tofauti kabisa wa uchezaji. Doncic ni fundi wa mashambulizi, anayedhibiti kasi ya mchezo, kutengeneza nafasi za kufunga akiwa na mpira na kuumiza ulinzi wa wapinzani akiwa karibu na eneo lolote la uwanja.
Kwa upande mwingine, Wembanyama ni mpambanaji katika ushambuliaji na ulinzi, akiwa na uwezo wa kufunga kwa urahisi huku akibadilisha kabisa namna timu pinzani zinavyoshambulia kutokana na urefu na uwezo mkubwa wa kusoma mchezo katika eneo la ulinzi. Hata hivyo, bado ni mapema mno kumtangaza mmoja wao kuwa ndiye anayependekezwa zaidi kushinda tuzo ya MVP.
Tuzo hiyo haiamuliwi kwa kuangalia takwimu binafsi pekee. Mafanikio ya timu, uwezo wa mchezaji kushiriki katika mechi nyingi kwa msimu mzima na mchango wake kwa ujumla katika matokeo ya timu yake pia vinakuwa na uzito mkubwa. Hata hivyo, nyota hao wawili tayari wameanza kutoa sababu za msingi za kuingia katika orodha ya wagombea wakuu wa tuzo hiyo.
Katika upande mwingine, kuna jambo jingine linalostahili kufuatiliwa, ambalo ni kuendelea kutawala kwa wachezaji wa kimataifa katika mbio za kuwania tuzo ya MVP ya NBA. Katika misimu ya hivi karibuni, nyota wa kimataifa kama Nikola Jokic, Giannis Antetokounmpo na Shai Gilgeous-Alexander wametawala mjadala wa tuzo hiyo na kufanikiwa kuibeba.
Na sasa Doncic na Wembanyama wanaibuka kama wagombea wawili wakuu wanaoweza kuendeleza mwenendo huo. Bado haijafahamika nani atakayebeba tuzo ya MVP mwisho wa msimu, lakini jambo moja linazidi kuonekana wazi; inakuwa vigumu kufikiria kuwa mshindi ajaye wa tuzo hiyo atakuwa mchezaji aliyezaliwa Marekani.