EPL imefika patamu sasa
Muktasari:
- Liverpool ilikuwa timu pekee kubwa iliyopoteza jana kwenye Ligi Kuu England, huku Chelsea na Man United zikitakata.
London. Huku vita ya Ligi Kuu England ikiendelea leo kati ya Arsenal na Tottenham Hotspur, jana kocha wa Liverpool Arne Slot alipokea kichapo cha kwanza kuanzia amejiunga na timu hiyo.
Liverpool ilikuwa timu pekee kubwa iliyopoteza jana kwenye Ligi Kuu England, huku Chelsea na Man United zikitakata.
Liverpool ambayo awali ilikuwa imeshinda mechi zote tatu za Ligi Kuu England imepokea kichapo cha bao 1-0 toka kwa Nottingham Forest, kwa bao safi lililofungwa na Callum Hudson-Odoi.
Sasa Forest wamefikisha michezo minne bila kupoteza chini ya kocha Nuno Espirito Santo.
Huu umekuwa mchezo wa kwanza Forest wanashinda kwenye Uwanja wa Anfield baada ya kupita miaka 55, walipofanya hivyo Februari 1969.
Baada ya mchezo huo, Slot alisema kuna makosa ambayo wachezaji wake waliyafanya lakini anaamini kuwa wanaweza kurudi kwenye kasi yao kwenye michezo ijayo.
“Tunakubali kuna sehemu tumekosea na tunakwenda mazoezini kurekebisha na nataka kuwaambia kuwa tutarejea tukiwa na nguvu kubwa zaidi kwenye mechi zijazo,” alisema.
Jadon Sancho awika Chelsea
Baada ya kushindwa kuonyesha kiwango cha juu kwenye kikosi cha Manchester United, jana kiungo wa Chelsea Jadon Sancho alifanikiwa kuonyesha uwezo wa juu baada ya kutoa pasi ya bao lililofungwa na Christopher Nkunku kwenye mechi dhidi ya Bournemouth.
Huu ulikuwa mchezo wa Ligi Kuu England ambao Chelsea waliibuka na ushindi wa bao 1-0, huku Nkunku akifunga bao lake la nne msimu huu akiwa anatokea benchi.
“Tunafahamu kuwa ni lazima jezi zetu zichafuke, kuibuka na ushindi kwenye mchezo huu ni jambo ambalo kila mmoja alikuwa analisubiri, niwapongeze wachezaji wangu wote,” alisema kocha wa Chelsea Enzo Maresca.
Haaland tena
Erling Haaland ameendelea kuonyesha umwamba wake kwenye Ligi Kuu England baada ya kufunga bao lake la tisa msimu huu.
Man City jana ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Brentford kwenye mechi kali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Etihad.
Staa huyo ameweka rekodi ya kufunga mabao tisa ndani ya mechi nne za Ligi Kuu England baada ya jana kufunga mabao yote mawili.
City imeendelea kujiweka kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa imeshinda mechi zote nne za ligi hiyo ikiwa ndiyo pekee imeweza kufanya hivyo hadi sasa.
Man United yaenda nafasi ya kumi
Baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Southampton, timu hiyo chini ya kocha Erik ten Hag imesogea hadi nafasi ya kumi kwenye msimamo wa ligi.
Sasa Man United imeshinda michezo miwili kwenye ligi na kupoteza miwili ikiwa na pointi sita.