Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MFUPA MGUMU: Rekodi 20 ambazo zitangoja sana kuvunjwa Ligi Kuu England

Muktasari:

  • Lakini, hiyo ni rekodi tu iliyofikiwa kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England, ambako kuna rekodi kibao, zitakazochukua muda mrefu sana kuvunjwa.

LONDON, ENGLAND: STRAIKA, Erling Haaland amefunga hat-trick tatu ndani ya mechi nane na kuvunja rekodi ya nyuma iliyokuwa ikiongozwa na Michael Owen, aliyefunga idadi hiyo ya hat-trick tatu kwenye mechi 48.

Lakini, hiyo ni rekodi tu iliyofikiwa kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England, ambako kuna rekodi kibao, zitakazochukua muda mrefu sana kuvunjwa.


1. Mechi chache kwa mchezaji kufunga hat-trick tatu

Rekodi: Mechi 8 - Erling Haaland, 2022/23

Hii ni rekodi ya hivi karibuni zaidi. Straika Erling Haaland alitua England majira ya kiangazi mwaka 2022 na tangu wakati huo hajasimama kufunga. Hat -trick yake ya kwanza alifunga dhidi ya Crystal Palace kwenye mechi yake ya ne Man City, kisha aliyofuata alifunga dhidi ya Nottingham Forest kabla ya kumalizia na Man United hiyo ikiwa ndani ya mechi nane za kwanza Man City.


2. Kugongesha mwamba mara nyingi mechi moja

Rekodi: Mara nne 4 – Darwin Nunez (Liverpool vs Chelsea, Januari 31, 2024)

Darwin Nunez amekuwa akikosolewa kutokana na mwendelezo wake wa kushindwa kutumia nafasi za wazi anazopata kufunga mabao tangu alipotua Anfield. Straika huyo hafungi mabao kwa kiasi cha kutosha, lakini kwenye mechi moja ya Ligi Kuu England, aliingia kwenye rekodi ya kugongesha mwamba mara nyingi zaidi (nne) wakati Liverpool ilipokipiga na Chelsea, Januari mwaka huu.


3. Mechi nyingi mfululizo bila kupoteza

Rekodi: Mechi 49 – Arsenal (Mei 7, 2003 – Oktoba 24, 2004)

Ni Arsenal pekee ndiyo iliyocheza msimu mzima kwenye Ligi Kuu England bila ya kuonja machungu ya kupoteza, kitu ambacho hata Man City na ubora wao wote wameshindwa kufikia hiyo rekodi. Arsenal ilicheza mechi 38 bila ya kupoteza, kisha ikaendelea na msimu mwingine kwa mechi nyingine kadhaa na kufikia 49, ndipo ilipokwenda kupoteza kwenye mchezo ya 50 dhidi ya Man United.


4. Kucheza mechi nyingi mfululizo

Rekodi: Mechi 310 – Brad Friedel (Agosti 14, 2004 – Septemba 29, 2012)

Kutokana na vikosi vingi kutumia mtindo wa kuwachezesha wachezaji wao kwa zamu ili kuhakikisha wote wanakuwa fiti kwa wakati mmoja, rekodi ya kipa Brad Friedel imekuwa salama na haionekani kama itakwenda kuvunjwa kirahisi kwa siku za hivi karibuni. Kipa huyo alicheza misimu minane bila ya kupumzika katika vikosi vya Blackburn Rovers, Aston Villa na Tottenham Hotspur.


5. Pointi chache ndani ya msimu

Rekodi: Pointi 11 – Derby County (2007/08)

Derby itakuwa inaomba dua kila msimu kwenye Ligi Kuu England kuhakikisha kunakuwa na timu itakayopata pointi chache kuzidi walizopata wao (11) kwenye msimu wa 2007/08. Kwa hali ilivyo, rekodi hiyo ya Derby inaonekana wazi itaendelea kuishi kwa miaka kadhaa na huenda isivunjwe ndani ya miaka michache. Katika msimu huo, Derby ilipata ushindi mmoja tu, bao 1-0 dhidi ya Newcastle United.


6. Vipigo vingi mfululizo

Rekodi: Vipigo 20 - Sunderland

(2003 - 2005)

Licha ya kwamba Derby iliweka rekodi ya kuvuna pointi chache zaidi ndani ya msimu mmoja kwenye Ligi Kuu England, lakini timu iliyoweka rekodi ya kufungwa mara nyingi kwenye mechi mfululizo ni nyingine kabisa, Sunderland, iliyofungwa kuanzia 2003 hadi 2005 kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England. Walipoteza mara 15 katika msimu wa 2002-03 na waliporejea kwenye ligi 2005, wakapoteza tena.


7. Mchezaji mwenye umri mkubwa

Rekodi: Miaka 43 na siku 162 – John Burridge (Man City vs QPR, Mei 14, 1995)

John Burridge alikuwa kipa, hivyo haishangazi kuona ameweka rekodi hiyo ya kucheza mechi akiwa na umri mkubwa zaidi kwenye Ligi Kuu England na hakika rekodi hiyo haijavunjwa na huenda ikadumu muda mrefu. Kipa huyo alicheza kwenye mechi baina ya Man City na Queens Park Rangers mwaka 1995 na kuweka rekodi ya kuwa uwanjani akiwa na umri wa miaka 43 na siku 162.


8. Ubingwa kwa tofauti chache ya pointi

Rekodi: Pointi 0 na tofauti ya mabao +8 (Man City, 2011/12)

“AGUUUERRRROOOOOO.” Sio tu ni kelele maarufu zaidi ya kutangaza goli kwenye Ligi Kuu England, bali pia iliweka rekodi ya kuipa ubingwa timu kwa tofauti ya pointi chache sana, (0) na chanya 8 ya tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa iliyopata Manchester City mbele ya mahasimu wao Manchester United. Hiyo ndiyo mara moja pekee bingwa wa Ligi Kuu alipatikana kwa tofauti ya mabao.


9. Bao la haraka zaidi

Rekodi: Sekunde 7.69 – Shane Long (Southampton vs Watford, Aprili 23, 2019)

Unaona kama haiwezekani bao kufungwa haraka hivyo kwa muda usiozidi sekunde saba kwenye Ligi Kuu England. Lakini, hilo lilifanywa na straika wa Southampton, Shane Long, ambaye alifunga kwenye sekunde ya saba tu ya mchezo wa ligi hiyo dhidi ya Watford, Aprili 2019. Alan Shearer, Dwight Yorke na Christian Eriksen walifunga mabao ya haraka, lakini hawajawahi kuvunja rekodi hiyo.


10. Bingwa wa ligi akiwa na pointi chache

Rekodi: Pointi 75 – Man United (1996/97)

Kutokana na Manchester City na Liverpool kuvuna pointi karibu 100 kwa misimu kadhaa ya hivi karibuni, utashangaa kwamba pointi 75 zimeshawahi kuifanya timu kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu England, ambayo ni Manchester United kwenye msimu wa 1996/97. Msimu wa 2017-18, Man City ilifikisha pointi 100, huku hizo pointi 75 zilifikiwa na timu iliyoshika nafasi ya nne, ambao ni Liverpool kwa wakati huo.


11. Mechi nyingi bila ya kupoteza nyumbani

Rekodi: Mechi 86 – Chelsea (Machi 20, 2004 – Oktoba 5, 2008)

Mechi 86 bila ya kupoteza nyumbani hilo lilifanywa na Chelsea kwenye Uwanja wa Stamford Bridge kwenye mikikimikiki hiyo ya Ligi Kuu England. Rekodi hiyo ilidumu hadi Liverpool ilipokwenda kwenye uwanja huo mwaka 2008 na kumshuhudia Xabi Alonso akifunga kwa shuti la mbali, kufikisha mwisho rekodi hiyo ya kutopoteza kwenye mechi nyingi ikicheza kwenye uwanja wa nyumbani.


12. Kufunga hat-trick ya haraka

Rekodi: Dakika 2, sekunde 56 – Sadio Mane (Southampton vs Aston Villa, Mei 16, 2015)

Haaland anapaswa kuchukua somo hapa kutoka kwa Sadio Mane, ambaye aliweka rekodi ya kufunga mara tatu ndani ya mechi moja huku mabao yake yakitofautiana dakika 2 na sekunde 56 tu. Kwenye rekodi, hiyo ndiyo hat-trick iliyopigwa haraka zaidi kwenye michuano ya Ligi Kuu England, ambapo hadi sasa haijavunjwa na huenda ikasubiri kwa miaka kadhaa kuvunjwa. Haaland ataweza?


13. Mechi nyingi bila ya kuruhusu bao

Rekodi: Dakika 1,113 - Edwin van der Sar (Man United, Novemba 15, 2008 – Februari 18, 2009)

Katika msimu wa 2008-09, Van der Sar alicheza mechi 14 bila ya kuruhusu bao kwenye nyavu zake na mechi hizo amecheza mfululizo. Rekodi hiyo ilikwenda kuvunjwa na staa wa Blackburn, Roque Santa Cruz. Rekodi ya kucheza mechi nyingi bila ya kuruhusu bao huko nyuma ilikuwa inashikiliwa na Petr Cech, ambaye kipa huyo wa Chelsea, alicheza kwa dakika 1,025 bila ya kuokota mpira nyavuni.


14. Kufunga bao kwa misimu mfululizo

Rekodi: Misimu 21 – Ryan Giggs (1992/93 - 2012/13)

Akicheza misimu 21 kwenye Ligi Kuu England, winga Giggs aliweka rekodi ya kufunga kwenye misimu 23 mfululizo. Giggs alifunga kwenye misimu miwili ya kwanza mfululizo kabla ya kuanza kwa mfumo wa sasa wa Ligi Kuu England mwaka 1992, ambapo aliendelea kufunga kwa kila msimu hadi 2012/13, ambao ulikuwa msimu wake wa mwisho, ambao staa huyo alifunga bao moja. Alicheza msimu mmoja tu bila ya kufunga ambao ulikuwa wa mwisho Man United 2013-14.


15. Kufunga mabao mengi kipindi kimoja

Rekodi: Mabao 5 – Jermain Defoe (Tottenham vs Wigan, Nov 22, 2009)

Hii ni rekodi nyingine ambayo itasubiri muda mrefu kuvunjwa kwenye Ligi Kuu England. Cole Palmer wa Chelsea nusura avunje rekodi hiyo wikiendi iliyopita, lakini aliishia kufunga mara nne tu, huku Defoe, akiendelea kubaki kwenye rekodi yake ya kufunga mara tano ndani ya kipindi kimoja, wakati Spurs ilipochapa Wigan 9-1 kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England.


16. Kocha  aliyedumu muda mrefu

Rekodi: Miaka 21, siku 224 – Arsene Wenger (Oktoba 1, 1996 – Mei 13, 2018)

Pep Guardiola ndiye kocha aliyedumu miaka mingi kwenye Ligi Kuu England kwa sasa kwa ambao wapo kwenye ligi hiyo baada ya Jurgen Klopp kuachana na Liverpool mwishoni mwa msimu uliopita. Lakini, rekodi ya jumla ya kocha aliyedumu kwenye Ligi Kuu England kwa miaka mingi inashikiliwa na kocha Wenger, aliyedumu Arsenal kwa miaka 21 na kumpiku Sir Alex Ferguson wa Man United.


17. Kufunga mara nyingi mfululizo dhidi ya timu moja

Rekodi: Mechi 9 - Sadio Mane vs Crystal Palace)

Achana na rekodi ya Luis Saurez dhidi ya Norwich City, rekodi ya kuifunga timu moja mara nyingi mfululizo kwenye Ligi Kuu England inashikiliwa na Sadio Mane dhidi ya Crystal Palace, ambapo amefunga kwenye mechi tisa mfululizo, wakati huo alipokuwa akikipiga Liverpool. Suarez aliifunga Norwich kwenye mechi tano mfululizo kiasi cha mabao 12. Lakini, Mane amefunga mechi tisa.


18. Kufungwa mabao machache ndani ya msimu

Rekodi: Mabao 15 – Chelsea (2004/05)

Kwa kuwa na kipa Petr Cech na safu ya ulinzi ya mabeki John Terry, Ricardo Carvalho, William Gallas na Paulo Ferreira, Chelsea chini ya kocha Jose Mourinho ilifungwa mabao machache sana katika msimu wa 2004/05, ambapo iliruhusu wavu wao kuguswa mara 15 tu, sawa na mabao 0.37 kwa kila mechi. Tangu kipindi hicho, hakuna timu nyingine kwenye Ligi Kuu England iliyoruhusu mabao machache.


19. Kufunga haraka baada ya kutoka benchini

Rekodi: Sekunde 6 – Nicklas Bendtner (Arsenal vs Tottenham, Desemba 22, 2007)

Nani atajitangaza kuwa mmaliziaji mzuri kumzidi Nicklas Bendtner kwa rekodi hii? Straika huyo akiwa Arsenal, aliweka rekodi ya kufunga bao haraka zaidi tangu alipoingia akitokea benchi na alifanya hivyo kwenye mechi dhidi ya mahasimu wao wa North London derby, Tottenham Hotspur. Bendtner hakutamba sana kwenye kikosi cha Arsenal na kuondoka kwa sababu timu ilikuwa na wakali Robin van Persie na Emmanuel Adebayor.


20. Kufungwa mabao mengi ndani ya msimu

Rekodi: Mabao 104 – Sheffield United (2023/24)

Rekodi ya kufungwa mabao mengi zaidi huko nyuma ilikuwa ya mabao 100. Swindon Town ndiyo iliyokuwa ikishikilia rekodi hiyo katika msimu wa 1992/93 kabla ya Sheffield United kuja kuivunja msimu uliopita kwa kuguswa mara 104.