Coutinho arejea, aungana na Neymar
Muktasari:
- Coutinho amejiunga na Santos hadi mwisho wa msimu huu ikiwa ni miezi sita baada ya kuondoka katika klabu yake ya utotoni, Vasco da Gama, akieleza kuwa alikuwa akipitia changamoto za kiafya na kiakili.
BRASILIA, BRAZIL; KIUNGO wa zamani wa Liverpool na Barcelona, Philippe Coutinho, mwenye umri wa miaka 34, amejiunga na Santos ya Brazil na hivyo kuungana tena na nyota mwenzake wa zamani wa timu ya taifa, Neymar Jr.
Coutinho amejiunga na Santos hadi mwisho wa msimu huu ikiwa ni miezi sita baada ya kuondoka katika klabu yake ya utotoni, Vasco da Gama, akieleza kuwa alikuwa akipitia changamoto za kiafya na kiakili.
Mchezaji huyo aliashiria uhamisho huo kwa kupiga picha pamoja na Neymar, huku wawili hao wakirejea katika picha yao ya zamani wakiwa katika kikosi cha vijana cha timu ya taifa ya Brazil.
Akizungumza kwa mara ya kwanza akiwa mchezaji wa Santos, Coutinho alithibitisha kuwa Neymar alikuwa na nafasi kubwa katika uamuzi wake wa kujiunga na klabu hiyo.
“Neymar alicheza nafasi muhimu sana katika kuja kwangu hapa. Ni mchezaji ambaye hahitaji utambulisho, ni rafiki yangu tangu utotoni na nafikiri alikuwa mtu wa kwanza kutoka katika ulimwengu wa soka kunitumia ujumbe baada ya mimi kuondoka Vasco,” alisema Coutinho.
“Siku iliyofuata tayari alikuwa amenitumia ujumbe, lakini wakati huo nilimwambia ‘Ney, itakuwa furaha kucheza na wewe, lakini kwa sasa sijisikii vizuri, haiwezekani.’ Kwa kweli, wakati huo haikuwa na maana kwangu kufanya hivyo.”
Coutinho alisema miezi kadhaa baadaye Neymar aliwasiliana naye tena, lakini bado alimpa jibu lilelile.
“Baada ya miezi kadhaa aliwasiliana nami tena, lakini jibu langu lilikuwa lilelile. Kisha wiki mbili zilizopita alinitumia ujumbe mwingine. Ndipo nikajiuliza, nikafikiria upya mambo yote. Nilitaka kurudi kucheza soka na nikajiuliza ‘kwa nini nisiende?’
“Ninakwenda katika klabu kubwa, katika jiji lingine. Isingekuwa haki kwangu kushindwa kurejea kazini na kushindwa kurejea kucheza soka.
“Nataka kumshukuru rais, Mattos na Ney. Nina furaha kukubali changamoto hii.”
Coutinho aliondoka Vasco akiwa amechoka kiakili, ambapo alitangaza mapema mwaka huu akisema alikuwa “amechoka sana kiakili” katika ujumbe wa kihisia aliouandika kwenye mitandao ya kijamii.
Alikuwa amerejea Vasco kwa mkataba wa kudumu mwaka uliopita baada ya kuitumikia kwa muda kwa mkopo akiwa Aston Villa, na awali alionekana kuwa na uwezekano mkubwa wa kuendelea kubaki klabuni hapo. Hata hivyo, baada ya kuzomewa mara kadhaa na mashabiki wa klabu hiyo katika wiki zake za mwisho, alitambua kuwa ulikuwa wakati muafaka kwake kusitisha kwa muda shughuli zake za kucheza soka.
Akiwa Liverpool, Coutinho alicheza mechi 152 na kufunga mabao 41.