Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Conte awachana Man United

Muktasari:

  • Kauli hiyo ya Conte imekuja baada ya jina lake kuhusishwa kwa kiasi kikubwa na nafasi ya ukocha wa Manchester United, kabla ya mabosi wa klabu hiyo kuamua kumpa kazi Mauricio Pochettino.

LONDON, ENGLAND: KOCHA Antonio Conte amewatupia dongo viongozi wa Manchester United akidai timu zinazohofia mbinu zake za kazi ndizo zinazokuwa na hofu ya kushinda mataji.

Kauli hiyo ya Conte imekuja baada ya jina lake kuhusishwa kwa kiasi kikubwa na nafasi ya ukocha wa Manchester United, kabla ya mabosi wa klabu hiyo kuamua kumpa kazi Mauricio Pochettino.

Conte, ambaye kwa sasa hana kazi baada ya kuondoka Napoli mwishoni mwa msimu wa kiangazi, alitajwa miongoni mwa makocha waliokuwa wakipewa nafasi ya kurithi mikoba ya Michael Carrick.

Hata hivyo, Manchester United iliamua kumchukua Pochettino, aliyekuwa akiinoa timu ya taifa ya Marekani, kwa gharama zilizoripotiwa kufikia pauni milioni 10 kama fidia.

Akizungumza katika kipindi cha podcast cha Cronache di Spogliatoio, Conte alionekana kutoridhishwa na taarifa zilizodai kuwa Manchester United ilimkwepa kutokana na ukali wa mbinu zake za ufundishaji na mahitaji makubwa kwa wachezaji.

Conte alisema kama kuna klabu inayoogopa mbinu zake, basi inaogopa pia kushinda, kwa kuwa mfumo wake wa kazi ndiyo unaozalisha matokeo.

Alisema anaona ni jambo la kushangaza kufikiria kuwa klabu kubwa kama Manchester United inaweza kuogopa falsafa inayolenga kuirejesha katika hadhi yake ya zamani.

Kocha huyo alikumbusha kuwa mara ya mwisho Manchester United kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England ilikuwa mwaka 2013 chini ya Sir Alex Ferguson.

Conte alifichua kuwa ana heshima kubwa kwa Ferguson, ambaye aliwahi kumtembelea nyumbani kwake jijini London na kupata nafasi ya kuzungumza naye kuhusu masuala ya soka.

Alisema Ferguson alifanikiwa kuifanya Manchester United kuwa klabu kubwa kupitia mbinu zake za kazi na kujituma, hivyo haoni sababu ya klabu hiyo kuogopa mfumo unaohitaji nidhamu na kufanya kazi kwa bidii.

Conte ameendelea kujijengea sifa ya kuwa kocha mwenye msimamo mkali na anayehitaji kiwango cha juu kutoka kwa wachezaji wake, licha ya rekodi yake nzuri ya kutwaa mataji.

Akiwa Chelsea, aliwahi kutofautiana na mshambuliaji Diego Costa, beki David Luiz pamoja na viongozi wa klabu hiyo.

Pia, aliondoka Tottenham mwaka 2023 baada ya mkutano mkali na waandishi wa habari, ambako aliwakosoa wachezaji wake kwa ubinafsi na kuhoji utamaduni wa klabu hiyo.

Napoli nako hakukaa muda mrefu baada ya kutwaa ubingwa wa Serie A, akieleza kuwa ndani ya klabu hiyo kulikuwa na mazingira ya chuki na uhasama.

Pamoja na misuguano hiyo, rekodi ya Conte kisoka inajieleza yenyewe. Amefanikiwa kutwaa mataji matano ya Serie A akiwa na Juventus, Inter Milan na Napoli, huku pia akitwaa Ligi Kuu England na Kombe la FA akiwa Chelsea.

Si mara ya kwanza kwa Conte kuzungumzia suala la kuhusishwa na Manchester United. Mwezi uliopita alikanusha taarifa zilizodai kuwa alikuwa ameweka masharti maalumu kabla ya kukubali kuinoa klabu hiyo.

Gazeti la La Repubblica, liliripoti kuwa Conte alitaka mamlaka makubwa katika usajili wa wachezaji na kuwa na nafasi ya meneja mwenye maamuzi ya mwisho, badala ya kuwa kocha mkuu anayefanya kazi chini ya mfumo wa kiufundi uliowekwa na wengine.

Hata hivyo, kupitia mitandao ya kijamii, Conte alikanusha taarifa hizo akisema jina lake limekuwa likihusishwa na klabu mbalimbali lakini hakuna mazungumzo yaliyofikia hatua ya mwisho.

Alisema baada ya kipindi kizuri na chenye mafanikio Napoli, anahitaji muda wa kutafakari kuhusu wakati sahihi wa kurejea kazini.

Conte alisisitiza kuwa taarifa kuhusu madai ya fedha, kutaka mamlaka kamili na hofu ya klabu dhidi ya tabia yake kali hazina msingi wowote kwa sasa.

Wakati Conte akiendelea kusubiri nafasi nyingine ya kazi, Pochettino tayari ameanza maisha yake mapya Manchester United.

Kocha huyo raia wa Argentina aliwasili Manchester baada ya kumaliza majukumu yake ya mwisho akiwa na timu ya taifa ya Marekani Jumanne, kabla ya kuongoza mazoezi yake ya kwanza Alhamisi.

Anatarajiwa kuiongoza United kwa mara ya kwanza katika mchezo mkubwa dhidi ya Liverpool utakaopigwa Uwanja wa Anfield Jumapili.

Pochettino anakabidhiwa jukumu hilo wakati Manchester United ikiwa katika eneo la hatari la kushuka daraja, ikiwa imeshinda mchezo mmoja pekee kati ya mechi zake 10 za mwanzo za Ligi Kuu England.