Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Majanga Bayern! Kane nje miezi kadhaa

Muktasari:

  • Kane, ambaye ni miongoni mwa washambuliaji tegemeo wa Bayern, alilazimika kuondoka uwanjani dakika ya 20 katika mchezo wa Bundesliga dhidi ya FC Cologne uliomalizika kwa sare ya mabao 1-1 kwenye Uwanja wa Allianz Arena.

MUNICH, UJERUMANI: KLABU  ya Bayern Munich imepata pigo kubwa baada ya mshambuliaji wake hatari, Harry Kane, kupata majeraha ya kifundo cha mguu yanayotarajiwa kumuweka nje ya uwanja kwa kipindi cha miezi kadhaa.

Kane, ambaye ni miongoni mwa washambuliaji tegemeo wa Bayern, alilazimika kuondoka uwanjani dakika ya 20 katika mchezo wa Bundesliga dhidi ya FC Cologne uliomalizika kwa sare ya mabao 1-1 kwenye Uwanja wa Allianz Arena.

Nyota huyo aliumia baada ya kukutana na beki Joel Schmied katika tukio la kuwania mpira. Ingawa beki huyo alifanikiwa kuucheza mpira, mwendelezo wa mguu wake ulimkuta Kane kwenye kifundo cha mguu.

Kane alijaribu kuendelea na mchezo baada ya kupatiwa matibabu, lakini hali ilionekana kuwa mbaya na hatimaye akalazimika kutolewa.

Mkurugenzi wa michezo wa Bayern, Max Eberl, alithibitisha kuwa mshambuliaji huyo amepata jeraha kwenye mishipa inayounganisha mifupa ya kifundo cha mguu.

Kupitia taarifa yake rasmi, Bayern ilisema vipimo vilivyofanywa na jopo la madaktari wa klabu hiyo vilibaini Kane amepata mpasuko wa mishipa kwenye kifundo cha mguu wa kushoto.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 33 atakosekana kwa miezi kadhaa, huku klabu ikimtumia salamu za kumtakia apone haraka.

Kukosekana kwa Kane ni pigo kubwa kwa Bayern, ikizingatiwa kuwa mshambuliaji huyo amekuwa na mchango mkubwa katika kikosi hicho baada ya kufunga mabao 10 katika mechi 16 alizocheza msimu huu.

Bayern pia inaendelea kukabiliwa na changamoto ya majeraha ya wachezaji wengine, akiwamo Luis Diaz, Saibari na Serge Gnabry.

Kana kwamba haitoshi, Michael Olise naye alilazimika kutolewa kipindi cha kwanza kilipokamilika kutokana na jeraha la sehemu ya mbele ya mguu. Bayern ilithibitisha kuwa Mfaransa huyo amepata mchubuko na atapatiwa matibabu katika siku zijazo.

Kocha Vincent Kompany, aliyerejea benchi kwa mara ya kwanza tangu kuanguka mwezi uliopita, amekiri kuwa sasa wachezaji wengine wanapaswa kujitokeza kuziba pengo la mastaa hao.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Kompany alisema wachezaji wa kiwango cha dunia kama Kane hawawezi kubadilishwa kirahisi, lakini kikosi chake kinapaswa kuonyesha nguvu ya pamoja.

Alisisitiza kuwa Bayern inahitaji kiwango cha juu kutoka kwa wachezaji ambao huenda bado hawajazoea presha kubwa ya kuitumikia klabu hiyo.

Kwa upande wa mchezo, Bayern ilijikuta nyuma baada ya mshambuliaji Mikey Moore, anayekipiga kwa mkopo kutoka Tottenham, kuifungia Cologne bao la kuongoza kipindi cha kwanza.

Nathaniel Brown aliisawazishia Bayern kabla ya mapumziko, lakini wenyeji walishindwa kupata bao la ushindi katika mchezo huo wa kwanza wa Kompany baada ya kurejea.

Matokeo hayo yameipa Borussia Dortmund nafasi ya kupanda kileleni mwa msimamo wa Bundesliga endapo itapata ushindi katika mchezo wake unaofuata.

Wakati huohuo, bado haijafahamika kama jeraha hilo litamfanya Kane kukosa robo fainali ya UEFA Nations League dhidi ya Norway mwezi Machi.

Kane alikuwa ametoka kuweka historia kwa kuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi katika historia ya timu ya taifa ya England, baada ya kufikisha mechi 126 katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Croatia.