Coastal yapata ushindi wa kwanza nyumbani, Maabad akiendeleza moto
Muktasari:
- Maabad alianza kuandika bao la kwanza dakika ya 10 kwa penalti, kabla ya JKT Tanzania kusawazisha dakika ya 45 kupitia Mohamed Otalo. Coastal ilirejea kwa nguvu kipindi cha pili na kupata bao la ushindi dakika ya 78 kupitia Shiza Kichuya kwa asisti ya Maabad na kuiwezesha timu hiyo kuondoka na pointi tatu.
COASTAL Union imepata ushindi wake wa kwanza wa Ligi Kuu Bara nyumbani msimu huu baada ya kuifunga JKT Tanzania mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, huku mshambuliaji wake, Maabad Maulid Maabad akihusika moja kwa moja katika mabao yote mawili ya timu hiyo.
Maabad alianza kuandika bao la kwanza dakika ya 10 kwa penalti, kabla ya JKT Tanzania kusawazisha dakika ya 45 kupitia Mohamed Otalo. Coastal ilirejea kwa nguvu kipindi cha pili na kupata bao la ushindi dakika ya 78 kupitia Shiza Kichuya kwa asisti ya Maabad na kuiwezesha timu hiyo kuondoka na pointi tatu.
Ushindi huo umekuja baada ya Coastal kuanza msimu kwa matokeo yasiyoridhisha. Ilipoteza nyumbani kwa bao 0-1 dhidi ya Mashujaa, ikafungwa 4-1 na Yanga ugenini, ikatoka sare ya 1-1 dhidi ya TRA United nyumbani na kupoteza ugenini 1-0 mbele ya Simba na kushinda mabao 1-2 ugenini dhidi ya Polisi Tanzania, kabla kuandika ushindi wake wa kwanza nyumbani dhidi ya JKT Tanzania kwa matokeo ya 2-1.
Maabad, ambaye aliibuka na tuzo ya mchezaji bora wa mchezo huo, ameweka wazi lengo lake msimu huu si kushindana na mshambuliaji mwingine, bali kuvunja rekodi yake mwenyewe ya mabao 10 aliyofunga msimu uliopita ambapo sasa amefikisha matatu.
“Mimi nashindana na rekodi mwenyewe. Msimu uliopita nilifunga mabao 10, lazima na msimu huu nivuke ili niivunje mwenyewe na tuzo yangu hii nampelekea mke wangu,” amesema Maabad, akionyesha wazi kwamba ana kiu ya kuongeza idadi hiyo kabla ya msimu kumalizika.
Huu ni muendelezo kwa mshambuliaji huyo ambaye mechi iliyopita dhidi ya Polisi Tanzania alifunga mabao yote mawili akiisaidia timu hiyo kuondoka na pointi tatu ugenini.
Kwa upande wa JKT Tanzania, Kocha Msaidizi, George Mketo, amesema timu yake ilijaribu kurejea baada ya kufungwa bao la mapema kwa penalti, lakini ikakosa umakini katika baadhi ya nyakati muhimu. Amesema pamoja na kipigo hicho, wanaamini mapumziko ya kalenda ya FIFA, yatakuwa nafasi ya kurekebisha upungufu uliobainika.
“Tumeumaliza mchezo salama, tulipofungwa goli la mapema la penalti tukarudi mchezoni. Matumaini yetu tutafanya vizuri zaidi kwenye mechi zijazo, lakini tunajutia kwa sababu tulikosa umakini,” amesema Mketo.
Kocha huyo amesema JKT Tanzania ina kikosi kizuri na wanatarajia kutumia kipindi cha mapumziko kuboresha maeneo yote ya timu ili kurejea ikiwa bora zaidi.
POLISI TZ 2-0 MBEYA CITY
Mbali na mchezo huo, mechi nyingine iliyopigwa mapema leo iliwakutanisha Polisi Tanzania iliyoondoka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City, ikichezwa kwenye Uwanja wa Usirika, Moshi mkoani Kilimanjaro.
Mabao yote mawili yalifungwa na mshambuliaji Anuary Jabir dakika ya 38 na 45.