Chelsea yamtaka John Stones
Muktasari:
- Mbali na Stones, Chelsea inaendelea na mazungumzo ya kumsajili beki wa Crystal Palace, Maxence Lacroix, huku pia ikimfuatilia beki wa Como, Jacobo Ramon, kama sehemu ya mpango wa kuimarisha safu ya ulinzi kabla ya kuanza kwa msimu mpya.
LONDON, ENGLAND: CHELSEA imeingia katika mbio za kumsajili beki wa kimataifa wa England, John Stones, kwa uhamisho wa bure baada ya mkataba wake na Manchester City kumalizika mwishoni mwa Juni.
The Blues sasa zinashindana na Inter Milan, ambayo pia inamuwania beki huyo mwenye umri wa miaka 32.
Mbali na Stones, Chelsea inaendelea na mazungumzo ya kumsajili beki wa Crystal Palace, Maxence Lacroix, huku pia ikimfuatilia beki wa Como, Jacobo Ramon, kama sehemu ya mpango wa kuimarisha safu ya ulinzi kabla ya kuanza kwa msimu mpya.
Wapanga kuwauza mabeki
Ili kutoa nafasi kwa wachezaji wapya, Chelsea pia inatarajia kuwaachia baadhi ya mabeki wake.
Beki wa England, Trevoh Chalobah, yupo kwenye mazungumzo ya kuhamia Como, huku Axel Disasi na Benoit Badiashile wakitajwa kuwa miongoni mwa wachezaji waliowekwa sokoni.
Stones ana historia kubwa City
Stones alijiunga na Manchester City akitokea Everton mwaka 2016 kwa ada ya pauni47.5 milioni na kucheza mechi 295 akiwa na mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu England.
Katika kipindi chake Etihad, alitwaa mataji sita ya Ligi Kuu, Ligi ya Mabingwa Ulaya, FA Cup mara mbili, Kombe la Ligi mara tano, Ngao ya Jamii mara tatu, Kombe la Dunia la Klabu pamoja na UEFA Super Cup.
Akiwa na timu ya taifa ya England, Stones amecheza mechi 93 na alikuwa sehemu ya kikosi kilichomaliza katika nafasi ya tatu kwenye Kombe la Dunia 2026.
Chelsea yaendelea kutikisa dirisha
Hatua ya kumuwania Stones inakuja siku chache baada ya Chelsea kutangaza rasmi usajili wa kiungo wa England, Morgan Rogers, kutoka Aston Villa kwa ada ya pauni milioni 117, ambayo ni rekodi mpya ya klabu.
Wakati huohuo, Chelsea inaendelea na mazungumzo na Aston Villa kuhusu uwezekano wa kumpeleka kwa mkopo winga wa Argentina, Alejandro Garnacho, kuelekea Villa Park.
Iwapo mazungumzo yatafanikiwa, Stones anaweza kuwa mmoja wa nyongeza muhimu katika kikosi cha Chelsea kinachojiandaa kupigania mataji msimu wa 2026-27.