Chelsea yamgeukia Granit Xhaka
Muktasari:
- Xhaka alicheza mechi 36 kwa Sunderland msimu uliopita, zikiwemo 34 za Ligi Kuu, na aliisaidia timu hiyo kumaliza nafasi ya saba na kufuzu kucheza UEFA Europa Ligi mara tu baada ya kupanda daraja kutoka Championship.
LONDON, ENGLAND: Chelsea imeanza mipango ya kutaka kufanya usajili wa kushangaza kwa kumleta kiungo Granit Xhaka kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.
Nyota huyo wa Uswisi mwenye umri wa miaka 33 alikuwa na msimu mzuri baada ya kurejea katika Ligi Kuu ya England akiwa na Sunderland.
Xhaka alicheza mechi 36 kwa Sunderland msimu uliopita, zikiwemo 34 za Ligi Kuu, na aliisaidia timu hiyo kumaliza nafasi ya saba na kufuzu kucheza UEFA Europa Ligi mara tu baada ya kupanda daraja kutoka Championship.
Nahodha huyo wa zamani wa Arsenal ambaye aliwahi kuvuliwa unahodha na kocha Unai Emery kufuatia mgogoro wake na mashabiki kabla ya kujijenga upya chini ya Mikel Arteta, anaripotiwa kuwa tayari amekubaliana kwa maneno kuhusu masharti binafsi ya kujiunga na Chelsea.
Kwa mujibu wa taarifa zinadai kuwa Chelsea tayari imeanza mazungumzo na Sunderland katika jitihada za kufanikisha uhamisho huo.
Jaribio la kumsajili Xhaka linaashiria mabadiliko ya sera ya usajili ya Chelsea chini ya umiliki wa BlueCo. Awali klabu hiyo ilijikita zaidi katika kusajili vipaji vya vijana, huku ikipuuzia wachezaji wenye uzoefu mkubwa.
Mkakati huo haukuzaa matunda msimu uliopita, ambapo Chelsea ilimaliza katika nafasi ya 10 kwenye ligi.
Baada ya kumteua Xabi Alonso kuwa kocha mkuu, aliyewahi kufanya kazi na Xhaka katika Bayer 04 Leverkusen walipotwaa ubingwa wa Bundesliga na DFB-Pokal bila kupoteza mchezo hata mmoja, Chelsea imeelezwa kuwa sasa inalenga zaidi kuwasajili wachezaji waliothibitisha uwezo wao.
Hata hivyo, ripoti kutoka Italia zikidai Chelsea iko tayari kutoa pauni26 milioni ili kukamilisha usajili huo.
Xhaka, ambaye amecheza kila dakika katika kampeni ya Uswisi kwenye Kombe la Dunia hadi sasa, ataleta uzoefu mkubwa ambao wengi waliamini ulikosekana katika kikosi cha vijana cha Chelsea msimu uliopita.