Bernal azigonganisha Chelsea, Man United
Muktasari:
- Bernal, ambaye alilelewa katika akademi maarufu ya Barcelona, La Masia, ameendelea kuonyesha maendeleo makubwa katika soka na tayari ameitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Hispania.
LONDON, ENGLAND: CHELSEA na Manchester United zimeingia kwenye mbio za kumsajili kiungo chipukizi wa Barcelona, Marc Bernal, huku Chelsea ikitajwa kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kumnasa nyota huyo mwenye umri wa miaka 19.
Bernal, ambaye alilelewa katika akademi maarufu ya Barcelona, La Masia, ameendelea kuonyesha maendeleo makubwa katika soka na tayari ameitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Hispania.
Hata hivyo, mustakabali wake ndani ya kikosi cha Barcelona umeanza kuwa na mashaka kutokana na ushindani mkubwa wa nafasi katika eneo la kiungo.
Barcelona hivi karibuni ilikamilisha usajili wa kiungo Rodri kutoka Manchester City, jambo ambalo limeongeza ushindani katika eneo hilo na huenda likapunguza nafasi ya Bernal kupata muda wa kutosha wa kucheza katika kikosi cha kwanza.
Hali hiyo imeifanya Chelsea kuchangamkia fursa hiyo, huku kocha wake Xabi Alonso akitajwa kuwa anamhitaji Bernal kama sehemu ya mipango yake ya muda mrefu.
Alonso anaamini Bernal ana uwezo wa kudhibiti kasi ya mchezo, kusambaza mipira kwa usahihi na kusaidia timu kujenga mashambulizi kuanzia eneo la chini la uwanja.
Chelsea pia inatafuta suluhisho la muda mrefu katika safu ya kiungo baada ya Enzo Fernandez kuondoka na kujiunga na Manchester City. Alonso anaamini Bernal anaweza kuwa mrithi wa muda mrefu wa kiungo huyo wa Argentina.
Kwa upande wa Manchester United, klabu hiyo imekuwa ikifuatilia maendeleo ya Bernal kwa muda na inamwona kama mchezaji anayefaa katika mpango wake wa kujenga upya safu ya kiungo kwa miaka ijayo.
Taarifa zinaeleza Chelsea tayari imeanza maandalizi ya awali kwa kuwasiliana na wawakilishi wa Bernal, huku ikimshawishi kwamba kuhamia London kutakuwa hatua muhimu katika maendeleo ya kipaji chake.
Mbio hizo zinatarajiwa kuwa kali zaidi kuelekea dirisha la usajili la Januari, huku Barcelona ikikabiliwa na changamoto za kifedha ambazo zinaweza kuifanya klabu hiyo kusikiliza ofa kubwa.
Hata hivyo, Barcelona bado ina nia ya kuwalinda wachezaji wake waliotokea La Masia.
Kwa sasa Chelsea inaonekana kuwa mbele ya Manchester United katika mbio hizo, lakini mustakabali wa Bernal unaweza kubadilika kabla ya dirisha la Januari kufunguliwa.