Bayern, Ajax kufungua uwanja mpya wa Talanta Kenya
Muktasari:
- Mchezo huo unatarajiwa kuipa Kenya fursa ya kuonyesha uwezo wake wa kuandaa mashindano makubwa ya kimataifa, huku ukitarajiwa kuvutia mashabiki wa soka kutoka sehemu mbalimbali za Afrika na duniani.
NAIROBI, KENYA: VIGOGO wa soka barani Ulaya, Bayern Munich ya Ujerumani na Ajax Amsterdam ya Uholanzi, wanatarajiwa kukutana Januari 5, 2027, katika mchezo maalumu wa ufunguzi wa Uwanja wa Kimataifa wa Raila Odinga uliopo katika eneo la Talanta Sports City jijini Nairobi, Kenya.
Rais wa Kenya, William Ruto, ametangaza mchezo huo utakaokuwa sehemu ya uzinduzi rasmi wa uwanja huo mpya wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000, ikiwa ni maandalizi ya nchi hiyo kuelekea fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kwa kushirikiana na Tanzania na Uganda.
Mchezo huo unatarajiwa kuipa Kenya fursa ya kuonyesha uwezo wake wa kuandaa mashindano makubwa ya kimataifa, huku ukitarajiwa kuvutia mashabiki wa soka kutoka sehemu mbalimbali za Afrika na duniani.
Bayern Munich, ambayo imetwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mara sita, itakuwa ikitembelea Kenya kwa mara ya kwanza. Kwa upande wa Ajax Amsterdam, klabu hiyo imejizolea umaarufu mkubwa barani Ulaya kutokana na historia yake ya mafanikio na kukuza vipaji vya vijana.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, timu hizo mbili zimekusanya jumla ya mataji 10 ya mashindano makubwa ya klabu barani Ulaya, jambo linaloufanya mchezo huo kuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wa soka.
Aidha, mchezo huo utakuwa sehemu ya maandalizi ya Ajax kwa ajili ya kurejea kwa mashindano ya msimu, wakati Bayern Munich itautumia katika kipindi cha mapumziko ya majira ya baridi ya Ligi Kuu ya Ujerumani.
Uwanja wa Kimataifa wa Raila Odinga, umejengwa kwa viwango vya kisasa na unatarajiwa kuwa miongoni mwa viwanja vitakavyotumika katika AFCON 2027, ambayo itaandaliwa kwa pamoja na Kenya, Tanzania na Uganda kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027.
Uwanja huo umeandaliwa kukidhi viwango vya CAF vya Kategoria ya Nne, huku ukiwa na sehemu maalumu za wageni waalikwa, pamoja na teknolojia za kisasa za kusaidia waamuzi katika mechi.
Mbali na soka, uwanja huo pia umeandaliwa kwa ajili ya kuandaa mashindano ya mchezo wa raga.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tiketi za mchezo huo zinatarajiwa kuanza kuuzwa Novemba 5, 2026, kupitia tovuti rasmi ya Talanta Sports City.
Uzinduzi huo unatajwa kuwa hatua muhimu kwa Kenya katika maandalizi ya AFCON 2027, huku ukitoa fursa kwa mashabiki wa Afrika Mashariki kushuhudia moja kwa moja baadhi ya majina makubwa ya wanasoka kutoka Ulaya akiwemo mshindi wa Ballon d'Or 2026, Harry Kane anayeitumikia Bayern Munich.