Somo la Tanzania Open kwa wenyeji
Muktasari:
- Ili kuzalisha mabingwa wa kimataifa, nchi inahitaji kuunganisha mashindano yenye ushindani, uwekezaji wa wadhamini na mfumo endelevu wa kukuza vipaji kuanzia ngazi ya vijana.
USHINDI wa Mmalawi Paul Chidale katika mashindano ya Vodacom Tanzania Open, umeacha ujumbe muhimu kwa mchezo wa gofu Tanzania.
Ili kuzalisha mabingwa wa kimataifa, nchi inahitaji kuunganisha mashindano yenye ushindani, uwekezaji wa wadhamini na mfumo endelevu wa kukuza vipaji kuanzia ngazi ya vijana.
Kwa misimu mitatu sasa, Tanzania haijawahi kutwaa ubingwa huo ambapo mara mbili umekwenda Kenya na safari hii nchini Malawi.
Msimu wa mwaka 2024, Greg Snow wa Kenya alishinda, huku nafasi ya pili ikishikwa na Mkenya mwingine, Sammy Mulama. Mwaka 2025, Mkenya, Joroge Kibugu alishinda na nafasi ya pili kuchukuliwa na John Lejirma ambaye pia ni Mkenya.
Chidale alitwaa ubingwa wa kitaalamu katika mashindano yaliyofikia tamati Oktoba 25, 2026 kwenye Uwanja wa Gofu wa Kili, Arusha, baada ya kutumia mipigo 289, moja juu ya kiwango cha kawaida cha uwanja, na kujinyakulia Sh9.35 milioni.
Ingawa taji hilo lilikwenda Malawi, mashindano hayo yameendelea kutoa jukwaa muhimu kwa wachezaji wa Tanzania kujipima dhidi ya washindani wa kimataifa, huku yakifungua mjadala kuhusu namna ya kugeuza fursa hizo kuwa maendeleo ya muda mrefu ya mchezo nchini.
Kwa Tanzania, mafanikio ya gofu hayawezi kupimwa kwa matokeo ya bingwa pekee, bali pia kwa idadi ya vipaji vinavyoibuka, ubora wa ushindani wa ndani na uwezo wa wachezaji kuendelea hadi kufikia kiwango cha kitaalamu.
MOLLEL AONYESHA NJIA
Mtanzania Nuru Mollel alitoa ushindani mkubwa kwa kumaliza nafasi ya pili kwa mikwaju 293, minne nyuma ya Chidale. Mkenya Robinson Owiti alishika nafasi ya tatu kwa mikwaju 294.
Matokeo ya Mollel yana umuhimu katika tathmini ya maendeleo ya wachezaji wa nyumbani. Mwaka 2025 alimaliza nafasi ya nne kwa mikwaju 305, hivyo kupanda hadi nafasi ya pili mw aka huu kuna onyesha hatua aliyopiga katika ushin dani huo.
Hata hivyo, tofauti ya mikwaju minne inaonyesha kuwa bado kuna nafasi ya kuboresha maandalizi, uthabiti wa kiwango na uwezo wa kutumia vizuri nafasi zinazopatikana katika raundi zote nne za mashimo 72.
Chidale alianza kwa mikwaju 73 akafuatiwa na raundi mbili za mikwaju 69 kabla ya kutumia 78 katika raundi ya mwisho. Licha ya kushuka kwa kiwango siku ya mwisho, matokeo yake ya awali yalitosha kumuhakikishia ushindi.
Kwa wachezaji wa Tanzania, ushindani wa aina hiyo ni fursa ya kujifunza namna ya kujenga faida, kudhibiti makosa na kudumisha umakini katika mashindano ya muda mrefu. Mollel na wachezaji wengine wa nyumbani wanahitaji kupata nafasi nyingi zaidi za kukabiliana na ushindani wa kiwango hiki ili kuimarisha uzoefu wao na kupunguza pengo lililopo.
MASHINDANO DARAJA LA KUKUZA VIPAJI
Vodacom Tanzania Open ina nafasi ya kuwa zaidi ya jukwaa la kutafuta bingwa wa kila mwaka. Inaweza kuwa sehemu ya mfumo mpana wa kukuza gofu, kuanzia vijana wanaojifunza mchezo huo hadi wataalamu wanaowania mataji makubwa.
Kuwepo kwa makundi ya wanaume, wanawake, vijana na wakongwe kunatoa nafasi kwa wachezaji wa viwango tofauti kushiriki na kupata uzoefu. Hata hivyo, matokeo ya muda mrefu yatategemea namna fursa hizo zinavyounganishwa na programu za maendeleo zinazofanyika mwaka mzima.
Chama cha Gofu Tanzania (TGU), klabu na wadau wa mchezo huo wanahitaji kuendeleza mashindano ya vijana, kuboresha upatikanaji wa makocha na vifaa, na kuweka njia zinazowawezesha wachezaji wenye vipaji kupanda kutoka ngazi za chini hadi ushindani wa kitaalamu.
Vilevile, wachezaji wanaoonyesha uwezo katika mashindano makubwa wanapaswa kusaidiwa kupata uzoefu zaidi kupitia mashindano ya ndani na ya kimataifa.
Bila mfumo huo, vipaji vinaweza kuonekana katika mashindano machache bila kupata maandalizi yanayohitajika ili kufikia kiwango cha juu.
UWEKEZAJI MUSTAKABALI WA GOFU
Jumla ya Sh40 milioni zimetumika kuwazawadia washindi katika mashindano yam waka huu kwa upande wa wachezaji wa kulipwa na Sh10 milioni kwa washindi wa mashindano ya ridhaa wenye viwango vya juu (Ellite Amateurs). Hii ni motisha kubwa kwa washiriki wa mashindano ya mwaka huu ambapo Chidale alipata Sh9.3 milioni, Mollel Sh6.3 milioni na Owiti Sh4.3 milioni.
Zawadi hizo zinaongeza ushindani na kuvutia wachezaji wenye uwezo, lakini mchango wa wadhamini unaweza kuwa mpana zaidi kupitia ushirikiano unaosaidia kukuza vipaji na kupanua ushiriki wa vijana.
Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando, alisema kampuni hiyo inatambua nafasi ya michezo katika kuunganisha watu, kukuza vipaji na kufungua fursa za mahusiano na ushirikiano.
Kauli hiyo inaonyesha umuhimu wa kuunganisha udhamini na malengo mapana ya maendeleo ya mchezo. Kwa gofu, hilo linaweza kumaanisha kuimarisha fursa za mafunzo, kusaidia mashindano ya vijana na kuongeza nafasi za wachezaji wa Tanzania kupata uzoefu wa ushindani wa hali ya juu.
“Uwekezaji wa Vodacom Tanzania katika mchezo wa gofu una lengo la kuendeleza mchezo na kufikia kiwango cha juu kabisa. Uwekezaji huu unaweza kusaidia kujenga msingi mpana wa wachezaji badala ya kutegemea mafanikio ya mtu mmoja au matokeo ya mashindano ya kila mwaka,” alisema Kamando.
USHINDANI WA KIMATAIFA UWE KIPIMO CHA MAENDELEO
Mwenyekiti wa TGU, Gilman Kasiga, amesisitiza umuhimu wa mashindano hayo katika kuendeleza mchezo na kuwapa wachezaji nafasi ya kupima uwezo wao dhidi ya washindani wa kimataifa kupitia mashindano ya Vodacom Tanzania Open.
Ushindani huo unatoa kipimo cha maendeleo ya wachezaji wa Tanzania na unaonyesha maeneo yanayohitaji kuboreshwa, kuanzia mbinu za kucheza hadi maandalizi ya kimwili na kisaikolojia.
Alisema kuwa mchezaji wa Kenya, Greg Snow alitwaa taji mwaka 2024, Njoroge Kibugu mwaka 2025 na Chidale mwaka huu, mabingwa hao wa kigeni wameendeleza mfululizo wa ushindi wa wageni. Hali hiyo haipaswi kuonekana kama sababu ya kukatisha tamaa, bali kama changamoto ya kuimarisha maandalizi ya wachezaji wenyeji. Kasiga alisema kuwa matokeo ya Mollel ya kumaliza katika nafasi ya pili, imetoa mfano wa maendeleo yanayoweza kujengwa kupitia ushindani. Kazi iliyobaki ni kuhakikisha kuwa hatua kama hiyo inakuwa sehemu ya mwenendo mpana wa wachezaji wengi zaidi wa Tanzania.
MAFANIKIO GOFU KWA MAENDELEO
Vodacom Tanzania Open imeendelea kuleta pamoja wachezaji, wadhamini na wadau wa gofu katika jukwaa la ushindani wa kimataifa. Lakini thamani yake ya muda mrefu itategemea pia kile kinachotokea baada ya kombe kukabidhiwa.
Ikiwa uzoefu unaopatikana katika mashindano hayo utaambatana na mafunzo bora, mashindano ya mara kwa mara na njia madhubuti za kukuza vipaji, Tanzania inaweza kujenga msingi imara zaidi wa ushindani.
Lengo si kusubiri tu siku ambayo mchezaji wa Tanzania atatwaa taji, bali kujenga mazingira yatakayowezesha wachezaji wengi zaidi kulipigania.