Mikonga katika mtihani mzito Zanzibar
Muktasari:
- Mbio hizo za ufungaji zitapata jibu lake mwisho wa msimu atakapopatika kinara wa ufungaji.
MFUNGAJI Bora wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) msimu uliopita 2025-2026, Tariki Mohammed Mikonga, ana mtihani mzito wa kuhakikisha alichokifanya awali, anakiendeleza.
Hata hivyo, kazi si nyepesi kwani katika raundi nane za ligi hiyo zilizochezwa msimu huu, mshambuliaji huyo wa JKU amezidiwa mabao matatu na kinara, Salum Akida wa Polisi.
Katika msimu huu wa 2026-2027, ushindani wa kuwania ufungaji bora umeanza kushika kasi.
Akida ambaye ni kinara, ana mabao matano na asisti moja, wakati mfungaji bora wa msimu uliopita, Tariki Mohamed Mikonga akiwa nayo mawili na asisti nne.
Kwa upande mwingine, Baktash Ali Bakari wa Muembe Makumbi ameanza msimu vizuri, akiwa amefunga mabao manne na kushika nafasi ya pili. Idadi hiyo ya mabao ni sawa na Rashid Salim wa Zimamoto, hali inayodhihirisha jinsi ushindani ulivyo mkali.
Kasi hiyo ya ufungaji inadhihirisha kwamba Akida ana kazi kubwa ya kuendelea kulinda nafasi yake ya uongozi, kutokana na washambuliaji wanaomfuatia kuwa karibu naye kwa idadi ya mabao.
Ikumbukwe kuwa, wakati Mikonga akiwa mfungaji bora msimu wa 2025-2026, alifunga mabao 22 na asisti moja, akiwa sawa na Michael Joseph, aliyekuwa akiichezea KVZ kabla ya kujiunga na Mashujaa anayoitumikia kwa sasa.
Msimu huo, nafasi ya tatu ilichukuliwa na James Mlange, aliyekuwa akiichezea Fufuni na sasa yupo Mafunzo, baada ya kufunga mabao 15. Kiungo wa kati wa Kipanga, Muslih Simai, alimaliza katika nafasi ya nne akiwa na mabao 14.
Wachezaji wengine watatu walimaliza msimu wakiwa na mabao 13 kila mmoja. Wachezaji hao ni Haji Makame wa KMKM, Faki Mwalimu wa Chipukizi na Baktash Ali Bakari, aliyekuwa akiichezea KMKM kabla ya kujiunga na Muembe Makumbi.
Mbio hizo za ufungaji zitapata jibu lake mwisho wa msimu atakapopatika kinara wa ufungaji.