Badu: Ghana tuna nafasi ya kufanya vizuri WAFCON
Muktasari:
- Ghana ilianza vizuri mashindano hayo baada ya kuifunga Cape Verde mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza, lakini ikakumbana na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Cameroon Agosti 2.
NYOTA wa Ghana, Evelyn Badu amesema Black Queens bado wana nafasi ya kufanya vizuri katika fainali za WAFCON 2026 licha ya kupoteza mchezo wao wa pili dhidi ya Cameroon.
Ghana ilianza vizuri mashindano hayo baada ya kuifunga Cape Verde mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza, lakini ikakumbana na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Cameroon Agosti 2.
Matokeo hayo yameifanya Ghana kukusanya pointi tatu, sawa na Mali, huku Cameroon ikiwa tayari imefuzu baada ya kushinda michezo yake yote miwili.
“Bado tuna nafasi ya kufanya vizuri kwenye mashindano haya. Tunachohitaji sasa ni kushinda mchezo wetu wa mwisho na kuendelea kuamini katika uwezo wetu,” alisema Badu.
Mchezo huo dhidi ya Mali utakuwa wa kufa au kupona kwa Ghana, kwani Mali nayo ina pointi tatu baada ya kuifunga Cape Verde mabao 3-2 katika mchezo wake wa pili. Ushindi wa Ghana utaongeza nafasi ya kusonga mbele, huku matokeo ya mchezo huo yakitarajiwa kuamua timu itakayemaliza nafasi ya pili katika Kundi D.
“Tunapaswa kuwa makini, kutumia nafasi zetu na kupambana kwa dakika zote. Tunajua Mali ni timu nzuri, lakini tunaamini tuna uwezo wa kupata matokeo tunayoyahitaji."
Ghana itakutana na Mali Agosti 6 katika Uwanja wa Moulay Rachid,mchezo wa kuamua hatma yao WAFCON 2026, huku Badu akiamini bado safari yao haijaishia hapo.