Aucho ‘ndo basi tena’ The Cranes
Muktasari:
- Aucho amethibitisha uamuzi huo kupitia ujumbe maalumu wa kuwaaga mashabiki wa The Cranes aliouchapisha kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, akieleza kujivunia safari yake akiwa sehemu ya timu hiyo.
Kiungo Khalid Aucho ametangaza kustaafu kuichezea timu ya taifa ya Uganda, The Cranes, baada ya kuicheza mechi 77 tangu alipoanza kuitumikia Novemba 30, 2013.
Aucho amethibitisha uamuzi huo kupitia ujumbe maalumu wa kuwaaga mashabiki wa The Cranes aliouchapisha kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, akieleza kujivunia safari yake akiwa sehemu ya timu hiyo.
Kiungo huyo aliyewahi kuzitumikia Yanga na Singida Black Stars za Tanzania, amejivunia kuwa miongoni mwa wachezaji walioisaidia Uganda kurejea kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) baada ya kusubiri kwa miaka 38.
Katika ujumbe wake, Aucho ameeleza fahari yake ya kushiriki fainali tatu za AFCON, zilizofanyika mwaka 2017, 2019 na 2025, akiwa sehemu ya kikosi cha The Cranes katika mashindano hayo makubwa ya soka barani Afrika.
Katika salamu zake za shukrani, Aucho amelishukuru Shirikisho la Soka Uganda (FUFA) na viongozi wake kwa nafasi na ushirikiano alioupata katika kipindi chote alichoitumikia timu ya taifa.
Pia, amewashukuru makocha waliomfundisha, akiwemo Milutin ‘Micho’ Sredojevic, Sébastien Desabre, Johnathan McKinstry, Paul Put na Fred Kajoba, ambaye amefariki dunia.
Aidha, amewashukuru wachezaji wenzake pamoja na mashabiki wa Uganda kwa kuwa sehemu ya safari yake ya kimataifa, akitambua mchango wao katika kipindi chote alichovaa jezi ya The Cranes.