Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Victor Wanyama afunguka kuhusu kustaafu soka

Muktasari:

  • Akiwa na umri wa miaka 34, wengi wanaweza kudhani wakati umefika kwake kutundika daluga, lakini amesema yupo kwenye harakati za kusaka changamoto mpya katika ligi tofauti.

Kiungo wa zamani wa Harambee Stars, Victor Wanyama, amesema bado hajamaliza kucheza soka licha ya kutumikia mchezo huo kwa miaka 19 katika klabu mbalimbali, huku akiwa nje ya uwanja kwa takribani miezi .

Akiwa na umri wa miaka 34, wengi wanaweza kudhani wakati umefika kwake kutundika daluga, lakini amesema yupo kwenye harakati za kusaka changamoto mpya katika ligi tofauti.

Iwapo mambo yangeenda sawa, Wanyama angeendelea kubaki Scotland na klabu ya Dunfermline Athletic, timu ya Ligi Daraja la Kwanza nchini humo aliyojiunga nayo Machi 26 mwaka huu kwa mkataba wa miezi miwili. Aliikuta ikipambana kuepuka janga la kushuka daraja na alipoondoka bado ilikuwa ikihangaika kubaki kwenye ligi hiyo.

 “Nilikuwa na mpango wa kusalia Dunfermline, lakini hatukuweza kukubaliana juu ya masharti ya mkataba mpya. Kwa sasa natafuta klabu nyingine,” amesema Wanyama katika mahojiano kwenye kipindi cha SportOn! cha runinga ya NTV kinachoendeshwa na Bernard Ndong na James Wokabi.

Mwezi Juni, kocha wa Harambee Stars, Benni McCarthy, alimwita kwenye kikosi kwa ajili ya mechi ya kirafiki nchini Chad, lakini hakujiunga na timu kwa sababu za kibinafsi.

Kwa sasa, Wanyama anaugawa muda wake katika kutafuta klabu mpya na kuhudhuria kozi ya ukocha.

“Kozi ya ukocha ni ngumu na inahitaji umakini mkubwa,” amesema.

“Nataka nijitengenezee nafasi zaidi za maisha ya baadaye pindi nitakapoacha kucheza.”

Jumapili jioni alitua jijini Nairobi akitokea London na kesho yake alihudhuria matukio na vyombo vya habari yaliyoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) akiwa Balozi wa CHAN 2024, akishirikiana na Mrisho Ngassa (Tanzania) na Dennis Onyango (Uganda).

Wanyama, anayefahamika pia kama “Big Vic”, alicheza kwa miaka saba nchini England akizitumikia klabu za Southampton (2013–2016) na Tottenham Hotspur (2016–2020). Akiwa England, alicheza jumla ya mechi 194 (mechi 97 kwa kila klabu), ingawa hakuwahi kutwaa kombe lolote.

Mwaka 2020 alihamia CF Montreal ya nchini Canada akitafuta mafanikio, lakini licha ya kucheza mechi 133, hakuambulia taji lolote hadi mwaka 2024 alipoondoka. Machi mwaka huo alirejea Scotland na kusaini kwa muda mfupi kuichezea Dunfermline Athletic.

Kabla ya hapo, Wanyama alicheza kwa mafanikio akiwa Celtic (2011–2013), ambako alitwaa mataji mawili ya Ligi Kuu ya Scotland na Kombe la Scotland.

Katika ziara yake ya ubalozi wa CHAN nchini Kenya, Wanyama alipeleka kombe jipya la michuano hiyo hadi Nation Centre na kulieleza kuwa “zito” likiwa na uzito wa takribani kilo sita au nane.

Alitabiri fainali ya michuano hiyo itazikutanisha timu za Morocco na Sudan, hata hivyo, fainali ambayo itachezwa Jumamosi Agosti 30 mwaka huu, Morocco itakabiliana na Madagascar, huku siku moja kabla Sudan ikicheza dhidi ya Senegal kuwania nafasi ya tatu.

Akizungumzia bonasi nono walizopewa wachezaji wa Harambee Stars baada ya kuishia robo fainali ya CHAN bila kupoteza mechi katika muda wa kawaida, Wanyama amesema: “Hiyo ndiyo njia ya kuwatendea wachezaji. Ukitoa stahiki kwa wakati na kwa heshima, wanajikita zaidi kupigania matokeo.”

Harambee Stars imemaliza michuano hiyo ikiwa na rekodi ya kucheza michezo mitano bila kupoteza ndani ya muda wa kawaida, ikishinda mitatu na sare miwili, kabla ya kutolewa kwa mikwaju ya penalti na Madagascar hatua ya robo fainali, mechi iliyochezwa kwa dakika 120 na matokeo kuwa 1-1.