Mtu nyuma ya glavu: Heshima kwa Albert Matitu, gwiji wa ndondi aliyejenga mabingwa
Msimamizi mkongwe wa ndondi Albert Matitu, aliyeaga dunia akiwa na umri wa miaka 74, atazikwa huko Ahero, Kaunti ya Kisumu, Jumamosi, Septemba 6, 2025.
Muktasari:
- Matitu ameacha historia kubwa katika ndondi hasa ndani ya Chama cha Ndondi cha Jeshi la Kenya (DEFABA), ambapo alifanya kazi akiwa kocha mkuu wa Shirikisho la Ndondi Kenya (BFK) hadi kifo chake.
ALIYEKUWA kocha maarufu wa ngumi Kenya, Albert Matitu aliyefariki wiki iliyopita akiwa na umri wa miaka 74, atazikwa Jumamosi, Septemba 6, 2025, katika kijiji cha Ahero, Kaunti ya Kisumu nchini humo.
Matitu ameacha historia kubwa katika ndondi hasa ndani ya Chama cha Ndondi cha Jeshi la Kenya (DEFABA), ambapo alifanya kazi akiwa kocha mkuu wa Shirikisho la Ndondi Kenya (BFK) hadi kifo chake.
Miongoni mwa mabondia waliopitia mikononi mwake ni Chris 'Bingwa' Sande aliyeshinda medali ya shaba kwenye michezo ya Olimpiki ya Seoul, Korea Kusini 1988 katika uzani wa middleweight.
Michezo hiyo ya Seoul inabaki ya kihistoria kwa Kenya na Afrika, baada ya Robert Wangila Napunyi kushinda dhahabu ya kwanza ya ndondi kwa Kenya na Afrika nzima.
Kocha wa zamani wa DEFABA, Rogers Munala, anasema alipokuwa mchezaji mwaka 1984, Matitu na marehemu Charles Longisa walikuwa wakisimamia timu hiyo ya kijeshi.
Matitu alianza maisha yake ya ndondi katika Klabu ya Ndondi ya Kariobangi kabla ya kujiunga na kikosi cha mafunzo ya wanajeshi 'Kenya Defence Forces' (KDF) akiwa kocha.
Munala anasema, "Nilikuwa nikicheza katika uzani wa welterweight kama Sande kabla hajahamia light middleweight."
Katika michezo ya Olimpiki ya Los Angeles Marekani mwaka 1984, Kenya iliwakilishwa na mabondia 10, akiwemo Sammy 'Kigos' Mwangi (bantamweight), Augustus 'Roje' Oga (middleweight), na marehemu, James 'Demosh' Omondi (heavyweight) waliotokea DEFABA.
Munala alimtaja Oga kama bondia aliyekuwa na mtindo wa kipekee na mkali wa kupigana, asiyekuwa na woga wowote wa kazi yake.
Kocha huyo alikumbuka pia ushindani mkali katika uzani wa heavyweight kati ya Demosh, Charles Amugune na Michael Boet, huku Kigos akipambana na bingwa wa taifa wa bantamweight, Peter Kimani na kukoleza vita alipojiunga na David 'Harish' Ouma kutoka nje ya jeshi.
Katika kikosi cha 'Hit Squad' cha 1988, kilichoenda Seoul, mbali na Sande, mabondia wengine wa DEFABA walikuwa, Anthony 'Scorpion' Ikegu (flyweight) na David 'Wonderboy' Wacheru, aliyeanza safari yake ya kimataifa kwenye mashindano ya Afrika mwaka 1979 na kushinda medali ya fedha.
Matitu aliteuliwa kocha mkuu wa Hit Squad katika michezo ya jumuia ya madola mwaka 1998 na Olimpiki za Athens 2004, kisha akawa meneja wa timu hiyo katika jumuia ya madola ya 2010, huko New Delhi India, Glasgow Scotland (2014) na ya Uingereza 2022.
Katika mashindano ya 1998 mjini Kuala Lumpur, Kenya ilinyakua medali mbili za fedha kupitia Moses Kinyua (light flyweight) na Absalom Okoth (welterweight) na medali moja ya shaba kupitia kwa Samuel Odindo (light heavyweight).
Kinyua, ambaye sasa anaishi Uingereza, amesema: "Matitu alikuwa pembeni yangu niliposhinda medali ya fedha. Nilifurahia Malaysia sana, hata kama sikushinda dhahabu."
Katika mashindano ya India 2010, Benson Gicharu alipata medali ya fedha (flyweight), huku Nick Okoth akitwaa medali ya shaba (bantamweight).
Shirikisho la Ndondi Kenya (BFK) liliomboleza kifo cha Matitu, kwa kusema, "Matitu alijitolea maisha yake yote kwa kukuza ndondi nchini Kenya, akihudumu kwa heshima, uadilifu, na ari kubwa kwa miaka mingi," ilieleza taarifa hiyo.
BFK liliongeza mchango wake kwa ndondi na malezi ya mabondia, makocha, na maafisa utaacha alama ya kudumu katika jamii ya ndondi.
"Tunaungana na familia yake, marafiki na jumuiya nzima ya ndondi katika kipindi hiki kigumu," ilieleza taarifa hiyo ya BFK.