Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Infantino kuhudhuria fainali ya CHAN, Madagascar vs Morocco Kenya

Muktasari:

  • Infantino ataungana na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe, pamoja na marais wa mashirikisho 54 ya mpira wa miguu barani Afrika kushuhudia fainali hiyo kati ya Morocco na Madagascar.

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino, anatarajiwa kuwasili nchini Kenya Jumamosi, Agosti 30 mwaka huu, kwa ajili ya kushuhudia fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) itakayopigwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Moi, Kasarani.

Infantino ataungana na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe, pamoja na marais wa mashirikisho 54 ya mpira wa miguu barani Afrika kushuhudia fainali hiyo kati ya Morocco na Madagascar.

Viongozi wakuu wa serikali ya Kenya akiwemo Rais William Ruto, Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga, Naibu Rais Kithure Kindiki, Waziri wa Michezo Salim Mvurya na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF), Hussein Mohammed, pia wanatarajiwa kuhudhuria.

Kuhudhuria kwa Infantino kunachukuliwa kama ishara ya kuonyesha imani na kuunga mkono uongozi wa soka nchini Kenya, hasa ikizingatiwa kwamba FKF imepita katika changamoto za uongozi zilizowahi kutishia mustakabali wa mpira wa miguu nchini humo.

Kwa kuwa mashindano ya CHAN 2024 yanachukuliwa kama majaribio kuelekea fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, ambazo Tanzania, Kenya na Uganda zitashirikiana kuandaa, ujio wa Infantino ni tamko la hadharani la kuthibitisha utayari wa Kenya kuandaa mashindano makubwa.

Tangu achaguliwe kuwa Rais wa FIFA, Infantino hajawahi kuzuru Kenya, na hii itakuwa mara yake ya kwanza. Hata hivyo, mwaka 2023 alihudhuria ufunguzi wa Ligi ya Soka Afrika (AFL) nchini Tanzania uliovutia mashabiki zaidi ya 60,000 ambapo Simba ilicheza dhidi ya Al Ahly.

Aidha, licha ya kutokanyaga nchini Kenya hapo awali, Infantino aliwahi kukutana na Rais wa FKF, Hussein Mohammed, katika hafla ya tuzo za CAF 2024 mjini Marrakech, Morocco.

Morocco, ambayo inaingia kwenye mchezo wa fainali kuwania taji lake la tatu la michuano hiyo, iliibuka na ushindi kwa mikwaju ya penalti 5-3 dhidi ya Senegal katika nusu fainali. Awali, iliitoa Tanzania kwa ushindi wa bao 1-0 kwenye robo fainali, baada ya kumaliza hatua ya makundi ikiwa nafasi ya pili nyuma ya Kenya kwenye Kundi A.

Kwa upande Madagascar ambayo imekuwa gumzo kwa safari yake ya kihistoria, ilimaliza nafasi ya pili nyuma ya Tanzania katika Kundi B na kufuzu robo fainali. Kisha ikaitoa Kenya kwa penalti 4-3, kabla ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Sudan kwenye dakika za nyongeza hatua ya nusu fainali, mechi iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kabla ya kuchezwa mechi ya fainali kuanzia saa 12:00 jioni, hafla kubwa ya kufunga mashindano imeandaliwa ambapo mashabiki wametahadharishwa kuingia uwanjani angalau saa tatu kabla ya mchezo kuanza ili kushuhudia burudani zote za kitaifa na kimataifa zitakazoambatana na tukio hilo.