Aussems amshangaa refa aliyemtupa jukwaani
KOCHA wa AFC Leopards, Patrick Aussems, hakuwa na maneno mazuri kuhusu mwamuzi aliyechezesha mchezo wa Ligi Kuu Kenya dhidi ya Posta Rangers Jumapili Uwanja wa Thika, kaunti ya Kiambu.
Katika mchezo huo ambao Ingwe walitoka nyuma na kushinda 3-1, Aussems alionyeshwa kadi nyekundi dakika chache kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika hivyo kulazimika kutizama kipindi cha pili akiwa jukwani.
Sababu iliyopeleka Aussems kutupwa jukwani ni kuvamia uwanjani akipinga mwamuzi kuchezesha zaidi ya dakika mbili zilizoonyeshwa na mwamuzi wa akiba na matokeo yake Posta Rangers wakapata bao la kuongoza lililofungwa na Calvin Odongo.
Akitumia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Aussems licha ya kumbwatukia refa huyo na hali ya Uwanja wa Thika, alisema ushindi wa Ingwe ni mahususi kwa shabiki kindakindaki wa timu hiyo, Isaac Juma, aliyezikwa Jumamosi kijijini kwao Mumias.
“Ningependa ushindi huu uende kwa Isaac Juma, shabiki namba moja wa Ingwe! Licha ya uwanja ambao haustahili kutumika kwa mechi za ligi kuu na refa ambaye hakuwa na uwezo, vijana walishinda kwa ajili yako! RIP Isaac,” aliandika Aussems.
Hata hivyo, kocha huyo wa Ingwe alisema ilikuwa aibu kitendo alichokifanya na kukiri alitawaliwa na hisia na angechukua njia bora zaidi kupata majibu kutoka kwa refa.
Kitu kingine kilichomkera Aussems ni hali ya uwanja licha ya timu yake kupata mabao matatu kipindi cha pili yaliyofungwa na Brian Wanyama, Washington Munene na Kayci Odiambo.
“Ni bahati mbaya Ligi Kuu ya Kenya inachezwa katika viwanja vibovu, mashabiki wanalipa kuja ili kupata burudani lakini inakuwa vigumu kwa wachezaji kuwapa burudani kwa aina ya uwanja,” alisema Aussems.
Mbali na Aussems aliyemlalamikia refa, mwingine ni nahodha wa Posta Rangers, Suleiman Ngotho, aliyedai Leopards walipewa penalti ya utata.
Ngotho alisema timu yake ilikua inafanya vizuri hadi refa alipohadaiwa na mashabiki wa Leopards na kuwapa penalti ambayo hawakustahili na kuwakatalia ya kwao iliyokuwa ya wazi.
Katika mechi hiyo, refa alikataa mabao mawili ya Ingwe na moja la Posta Rangers kwa madai wafungaji wa mabao yote walikuwa wameotea.