Zimamoto inabonda na kunyonga Ligi Kuu Zanzibar
Muktasari:
- Ushindi huo umeifanya Zimamoto kufikisha pointi 22, ikiwa na pengo la pointi nne dhidi ya Polisi, inayoshika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo.
ZIMAMOTO imeendelea kutanua wigo wa uongozi wake katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) baada ya kuichapa Mlandege mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika Oktoba 29, 2026 kwenye Uwanja wa Mao A, Unguja.
Shujaa wa Zimamoto alikuwa Ibrahim Hamadi, aliyefunga mabao yote mawili dakika ya 42 na 51, na kuiwezesha timu hiyo kuondoka na pointi tatu.
Ushindi huo umeifanya Zimamoto kufikisha pointi 22, ikiwa na pengo la pointi nne dhidi ya Polisi, inayoshika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo.
Katika michezo tisa ilizocheza, Zimamoto imeshinda saba, imepoteza moja na kutoka sare moja. Rekodi hiyo inaifanya kuwa timu iliyopata ushindi mwingi zaidi hadi sasa katika ligi hiyo.
Kwa upande wa Mlandege, kipigo hicho kimekatiza mwendo wake mzuri baada ya kushinda michezo miwili mfululizo. Matokeo hayo yameifanya kushuka hadi nafasi ya nane ikiwa na pointi 11.
Katika mchezo mwingine uliofanyika Uwanja wa Mao B, KMKM iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Uhamiaji, matokeo yaliyoifanya kufikisha pointi 13 na kupanda hadi nafasi ya saba.