ZILITRENDI: Mserbia acharukia uongozi wa Yanga

TAREHE kama ya leo ya Machi 24, lakini mwaka 2008 iliripotiwa taarifa ya Kocha Msernia, Dusan Kondic kuucharukia uongozi wa Yanga kwa madai ya kufanya mambo bila ya taratibu hali inayosababisha klabu hiyo kusajili wachezaji majeruhi.
Imeelezwa siku mbili kabla ya kwenda Libya ambako Yanga ilikuwa inacheza na Al Akhdar katika mechi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mwaka huo, Kondic alikaa na baadhi ya viongozi na kuwaeleza matatizo kadhaa likiwemo suala la usajili wa wachezaji bila kuwapima afya kitu ambacho kinampa wakati mgumu la machaguo ya wachezaji kulingana na mechi.
Pia kocha huyo alilalamikia tabia ya wachezaji wa timu hiyo hasa wale wanaotoka nje ya Tanzania kutojituma na kufanya asilimia kubwa kuanzia benchi au kukaa jukwaani kama watazamaji huku wakiendelea kula mshahara mnono.
"Kocha alicharuka sana, alitaka wachezaji kujituma na kuonyesha kweli wao wana malengo, alisisitiza kila atakayecheza katika kikosi chake ni yule ambaye ataonyesha anataka kufanya hivyo," kilisema chanzo hicho.
"Lakini alisisitiza viongozi ni chanzo pia kwa sababu walisajili wachezaji bila kufuata utaratibu wa kitaalamu," chanzo kilisema.
Anaamini kusajili wachezaji bila ya kuwapima afya ni tatizo kubwa, mfano kumbe (Aime) Lukunku kabla ya kuja Yanga alikuwa amevunjika mguu kitu kinachomfanya acheze kwa woga na Yanga kama wangempima wasingemsajili.
Takribani miezi minne iliyopita baada tu ya kutua nchini kwa ajili ya kuinoa Yanga, Kondic alichukua wachezaji wote na kuwapima afya, inaelezwa alikuta kuna upungufu mwingi na baadhi yao kama hawatapata nafuu watajumuishwa kwenye kundi la kuachwa msimu ujao.
Tayari James Chilapondwa kutoka Malawi na Laurent Kabanda kutoka DR Congo wapo kwao kwa ajili ya matibabu, majeruhi mwingine ni Vincent Barnabas ambaye inaaminika ni mchezaji ghali zaidi Yanga kwa wachezaji wa hapa nyumbani.
Alipoulizwa Kondic kwamba pamoja na kuwacharukia viongozi na wachezaji ana nini cha kufanya alisema; "Nina mechi ngumu dhidi ya Walibya, hicho ndicho kikubwa zaidi baada ya kurudi ninaweza kuzungumza mengine. "Lakini hata ukiangalia mwenyewe Yanga inapocheza unaona wachezaji wa kulipwa walio uwanjani ni wawili tu (Wisdom Ndhlovu na Maurice Sunguti) wengine ni majeruhi au kiwango chao kipo chini.
Katika mechi hiyo ya Libya, Yanga ililala bao 1-0 na iliporudiana nao nyumbani ilijitutumua na kutoka sare ya 1-1, lakini ikawaong'oa michuanoni kwa jumla ya mabao 2-1.