ZFF yajivunia Azam, Yanga kuutangaza Amaan Complex
Muktasari:
- Msimu wa 2024-2025, Simba iliutumia Uwanja wa New Amaan Complex katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch, kisha fainali ya michuano hiyo dhidi ya RS Berkane.
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), limeeleza kuridhishwa na namna Uwanja wa New Amaan Complex unavyoendelea kupata umaarufu kutokana na klabu kubwa zinazoutumia katika mechi za kimataifa, likisema hatua hiyo ni fursa muhimu kwa maendeleo ya soka Zanzibar.
Ofisa Habari wa ZFF, Namala Suleiman amesema Simba, Yanga na Azam zimekuwa miongoni mwa zinazochangia kuitangaza Zanzibar kutokana na matumizi ya uwanja huo katika mechi mbalimbali za kimataifa.
Namala amesema New Amaan Complex imekuwa hazina kubwa kwa soka la Zanzibar, kutokana na kuvutia michezo ya kiwango cha juu ambayo si tu inaupa uwanja huo heshima, bali pia inaongeza hamasa kwa wadau wa soka kisiwani hapa.
"Tunaendelea kushuhudia klabu kubwa ikiwemo Simba, Yanga na Azam kuutumia uwanja huo katika mechi za kimataifa, jambo ambalo linaleta faraja," amesema.
Msimu huu wa 2026-2027, Azam na Yanga zimeendelea kuuchagua uwanja huo kwa ajili ya mechi zao za kimataifa, jambo ambalo Namala amesema linachangiwa na ubora wa uwanja pamoja na maboresho makubwa yaliyofanyika katika miundombinu yake.
Amesema uwepo wa mechi hizo Zanzibar ni fursa kwa klabu za ndani kujifunza, kujenga hamasa na kuongeza juhudi katika kuimarisha ushindani ili nazo ziweze kufikia hatua ya kushiriki na kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
Namala alisisitiza klabu za Zanzibar zinapaswa kuwekeza katika maeneo mbalimbali, ikiwemo uimarishaji wa mifumo ya kiufundi na kiuchumi, ili kuwa na timu imara zinazoweza kushindana ndani na nje ya nchi.
Pia, aliwapongeza Simba, Yanga na Azam kwa kuendelea kuutumia New Amaan Complex na mechi zinazofanyika katika uwanja huo zina manufaa kwa wananchi kupitia shughuli mbalimbali za kibiashara zinazochochewa na uwepo wa mashabiki na wageni.
Amesema ZFF inaendelea kujifunza kutokana na fursa zinazotokana na matumizi ya uwanja huo, huku ikitamani kuona klabu za Zanzibar zikifanya vizuri zaidi katika mashindano ya kimataifa na kuipa heshima soka la visiwani hapa.
Msimu wa 2024-2025, Simba iliutumia Uwanja wa New Amaan Complex katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch, kisha fainali ya michuano hiyo dhidi ya RS Berkane.
Pia Singida Black Stars msimu uliopita 2025-2026, mechi zake zote za hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika ilicheza hapo sambamba na Azam na Yanga iliyokuwa Ligi ya Mabingwa Afrika.