ZFF yaanzisha Ligi ya viziwi Zanzibar
Muktasari:
- Mashindano hayo yatakayoshirikisha timu tano yanatarajiwa kuanza Septemba 17 hadi 27, 2026 katika viwanja vya Mao vilivyopo Mjini Unguja.
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Michezo ya Viziwi Zanzibar (SHIMIVIZA) wameandaa ligi ya visiziwi kisiwani hapa.
Mashindano hayo yatakayoshirikisha timu tano yanatarajiwa kuanza Septemba 17 hadi 27, 2026 katika viwanja vya Mao vilivyopo Mjini Unguja.
Akitambulisha michuano hiyo, Ofisa Habari wa ZFF, Namala Suleiman alisema mashindano hayo ni kipimo cha kutoa wachezaji wa timu ya Taifa ya viziwi Zanzibar.
“Mashindano haya yatatoa wachezaji watakaounda timu ya taifa ya viziwi Zanzibar kwa ajili ya mashindano ya kimataifa yatakayofanyika nchini Ethiopia,” alisema.
Alisema, ZFF imeamua kushirikiana na Shirikisho hilo kwa lengo la kuwapa nafasi wenye vipaji kuviendeleza kama ilivyo kwa wengine.
Pia, alisema wanahitaji kurejesha heshima kwa jamii kwa kuwasaidia kutimiza malengo yao kwani nao wanayonafasi hiyo.
Namala alisema, kwa kuanzia mashindano hayo timu tano zitashiriki na itachezwa kwa siku 10 hivyo wadau wa michezo wafike viwanjani kuzipa hamasa timu hiyo.