Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zanzibar Spice Boys bingwa Silver Cup katika mashindano ya PqCupBrazil

ZANZIBAR Pict

Muktasari:

  • Timu hiyo imepata ubingwa huo baada ya kuitembezea kichapo cha mabao 6-1, Amora Sports ya Brazil katika fainali iliyochezwa jana Oktoba 15, 2026 nchini Brazil.

TIMU ya Zanzibar Spice Boys imetwaa ubingwa wa Silver Cup katika mashindano ya kimataifa ya vijana ya PqCupBrazil 2026 yaliyofanyika nchini humo.

Timu hiyo imepata ubingwa huo baada ya kuitembezea kichapo cha mabao 6-1, Amora Sports ya Brazil katika fainali iliyochezwa jana Oktoba 15, 2026 nchini Brazil.

Mashindano hayo yaliyokuwa na sehemu tatu ikiwemo tuzo ya dhahabu (Gold), tuzo ya fedha(Silver) na tuzo ya shaba ( Bronze),  Zanzibar Spice imekuwa bingwa katika Silver Cup baada ya kutolewa katika kinyang'anyiro cha dhahabu kwenye hatua ya robo fainali ya mashindano hayo.

Kikosi hicho kinachoundwa na wachezaji chipukizi 18 wenye umri wa miaka 12 na 13 kutoka Dulla Sunday Academy, kimeandika historia kwa kutwaa ubingwa huo katika mashindano hayo ya kimataifa ya vijana.

Akizungumza baada ya ubingwa huo, mkuu wa msafara ambaye pia ni Balozi Mstaafu, Abdulsamad Abdulrahim, amesema mbali na kushiriki mashindano hayo ilikuwa fursa ya kuanzisha mawasiliano, kujenga uhusiano wa kimataifa pamoja na kuitangaza Zanzibar katika utalii na uwekezaji.

"Lengo ni kujenga mitandao inayozalisha fursa, kuimarisha uhusiano baina ya watu na kuvutia uwekezaji. Mpira wa miguu umetuleta hapa na ushirikiano wa kimkakati utazalisha fursa," amesema

Alisisitiza kuwa, mafanikio ya kweli ya safari hiyo hayatapimwa kwa kombe pekee, bali fursa zitakazofunguliwa na hatua zitakazochukuliwa kuwasaidia vijana kuendeleza vipaji vyao.

Timu hiyo, ilianza na sare 1-1 dhidi ya Juventude Sports kwenye hatua ya makundi ya mashidano hayo kisha ikaifunga Minas Gerais mabao 5-0 na mchezo wa mwisho wa makundi ikafungwa mabao 4-2 na Soccer Pro.

Katika hatua ya robo fainali, timu hiyo ilitembeza kipigo cha mabao 10-0 kwa timu ya Alcatéia Novo Horizonte lakini ikafungwa mabao 2-1 na E10 Soccer na kuondoshwa katika tuzo ya dhahabu na kuingia katika kinyang'anyiro cha Silver.

Kwenye hatua ya nusu fainali ya Silver Cup ya mashindano hayo Zanzibar Spice Boys iliifunga Rio Branco mabao 3-1 kisha ikamaliza kwa kuifunga Amora Sports mabao 6–1, ushindi ulioifanya timu hiyo kuwa bingwa wa Silver Cup.

Ushindi wa mabao 10-0 dhidi ya Alcatéia Novo Horizonte na ushindi wa fainali wa 6-1 ni miongoni mwa matokeo yaliyodhihirisha uwezo wa timu hiyo kufunga mabao na kucheza kwa dhamira ya kuitangaza Zanzibar.