Zanzibar kutumia vipaji kujitangaza AFCON 2027
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema itatumia vijana wenye vipaji vya soka katika shughuli za kuitangaza Zanzibar kimataifa, sambamba na maandalizi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), zitakazoandaliwa kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda.
Akizungumza kuhusu mpango huo, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Dk. Riziki Pembe Juma, amesema vijana ni miongoni mwa rasilimali muhimu katika kuitangaza Zanzibar kimataifa, hivyo Serikali itaendelea kuwaunga mkono ili kukuza vipaji vyao na kuleta manufaa kwa taifa.
Amesema maandalizi ya AFCON 2027 yanapaswa kutumiwa kama fursa ya kuonesha uwezo wa vijana, kukuza vipaji vyao na kuwafungulia milango ya kupata fursa za kimataifa.
Ameongeza kuwa Zanzibar ipo tayari kushirikiana na Tanzania Bara, Kenya na Uganda kuhakikisha mashindano hayo yanafanikiwa, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia fursa zitakazotokana na michuano hiyo kuendeleza michezo na kuwapa vijana nafasi ya kuonesha uwezo wao. Zanzibar tupo tayari kwa AFCON 2027.
“Tutumie nafasi hii vizuri, lakini pia tuhakikishe tunaendelea kukuza vipaji vya watoto wetu,” amesema.
Dk. Riziki amesema Serikali inaendelea na juhudi za kuendeleza michezo na kuwawezesha vijana kupata fursa za mafunzo nje ya nchi, akieleza kuwa juhudi hizo zinatarajiwa kuleta matokeo chanya baadaye.
Ameahidi kuwa Serikali itaendelea kushughulikia changamoto zinazoikabili sekta ya michezo kwa kushirikiana na taasisi husika ili kuboresha mazingira ya michezo na kuinua kiwango cha soka Zanzibar.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia na kuendeleza vipaji vilivyopo nchini ili kuhakikisha vijana wanapata nafasi ya kushiriki katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.