Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ZAA yajipanga kupokea wageni wa AFCON 2027, Zanzibar

ZAA Pict

Muktasari:

  • Ziara hiyo inalenga kuimarisha miundombinu na huduma za usafiri wa anga, afya na utalii ili kukidhi mahitaji ya wanamichezo, wageni na wananchi wakati wa michuano hiyo.

BODI ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA) imekagua maeneo mapya yaliyopendekezwa kwa ajili ya miradi ya miundombinu ya usafiri wa anga, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Zanzibar kuelekea Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Ziara hiyo inalenga kuimarisha miundombinu na huduma za usafiri wa anga, afya na utalii ili kukidhi mahitaji ya wanamichezo, wageni na wananchi wakati wa michuano hiyo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya ZAA, Juma Burhan, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga ili kuongeza ufanisi wa huduma na kuiwezesha Zanzibar kukabiliana na mahitaji yatakayojitokeza wakati wa maandalizi na uendeshaji wa AFCON 2027.

Amesema miundombinu hiyo itakuwa na mchango mkubwa katika kukabiliana na dharura za kiafya zinazoweza kuwakabili wanamichezo, wageni na wananchi, hasa pale itakapohitajika kuwasafirisha wagonjwa kwa ajili ya kupata matibabu ya haraka.

“Miundombinu hiyo itaimarisha uwezo wa Zanzibar kutoa huduma za usafiri wa anga na kukabiliana na mahitaji ya dharura yatakayojitokeza wakati wa michuano hiyo,” amesema Burhan.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa ZAA, Seif Abdalla Juma, amesema maendeleo ya miundombinu hiyo yatasaidia kuboresha huduma za usafiri wa anga na kuongeza fursa za kiuchumi kupitia utalii, uwekezaji na biashara.

Amesema maeneo hayo mapya yanatarajiwa kuanza kutoa huduma kabla ya kuanza kwa AFCON 2027, hatua inayolenga kurahisisha usafiri wa wageni, kuongeza thamani ya vivutio vya utalii na kuchochea shughuli za biashara.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Zanzibar za kuimarisha miundombinu na kukuza uchumi.

Katika ziara hiyo, viongozi hao walitembelea mradi wa uwanja wa ndege wa Makunduchi pamoja na maeneo yaliyopendekezwa kwa ajili ya kutua kwa helikopta katika Hospitali ya Lumumba, Fumba, Paje na Kizimkazi.

AFCON 2027 itakayofanyika Juni 19 hadi Julai 17, 2027, Tanzania itakuwa mwenyeji kwa kushirikiana na Kenya na Uganda. Kwa Tanzania, mechi zitachezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Samia Suluhu Hassan (Arusha) na Fumba (Zanzibar).