Zabona mlangoni TRA United
Muktasari:
- Nyota huyo aliyejiunga rasmi na Pamba Jiji, Desemba 14, 2024, akitokea Tanzania Prisons ya jijini, Mbeya, mkataba wake na kikosi hicho kutoka jijini, Mwanza unafikia tamati Januari 2027, huku kukiwa hakuna mazungumzo ya kuongeza mwingine.
TRA United iko katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa winga wa Pamba Jiji, Zabona Mayombya, wakati wa dirisha dogo la usajili wa Januari 2027, litakapofunguliwa rasmi, baada ya mkataba wake wa miaka miwili kufikia tamati.
Nyota huyo aliyejiunga rasmi na Pamba Jiji, Desemba 14, 2024, akitokea Tanzania Prisons ya jijini, Mbeya, mkataba wake na kikosi hicho kutoka jijini, Mwanza unafikia tamati Januari 2027, huku kukiwa hakuna mazungumzo ya kuongeza mwingine.
Taarifa kutoka ndani ya Pamba Jiji, zimeliambia Mwanaspoti mchezaji huyo alipewa mkataba mpya wa kuendelea kubakia na timu hiyo, japo amewataka mabosi wa kikosi hicho kusubiria ili afanye uamuzi, jambo ambalo limeibua wasiwasi kikosini.
Chanzo hicho kilisema wamepata taarifa za baadhi ya klabu kufanya mazungumzo na mchezaji huyo ya kutaka kumsajili katika dirisha dogo la Januari 2027, litakapofunguliwa, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kushindwa kuongeza mwingine.
“Mkataba wake unaisha Januari 2027 na tuliongea naye ili kumuongezea mwingine mmoja zaidi, ila mazungumzo ya pande mbili kati yetu hadi sasa hayajafikia sehemu nzuri, nadhani amefanya uamuzi wa timu mpya atakayoenda,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, Mwanaspoti inatambua nyota huyo amepata ofa nono ya kujiunga an TRA katika dirisha dogo la Januari 2027, jambo ambalo limekuwa gumu kwake kusaini mkataba mpya, baada ya kufikia makubaliano mazuri kati ya pande mbili.
Nyota huyo amekuwa mhimili mkubwa wa Pamba Jiji msimu huu wa 2026-2027, baada ya kufunga bao moja la Ligi Kuu Bara na asisti moja.
Kwa msimu wa 2025-2026, Zabona alitoa asisti nane za Ligi Kuu na kushika nafasi ya tatu kwa waliotoa nyingi zaidi, nyuma ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC aliyekuwa na tisa na Elie Mpanzu wa Simba aliyeongoza na 10.