Pamba Jiji yaendelea kusuasua Ligi Kuu
Muktasari:
- Ikiwa nyumbani, Pamba Jiji ilionekana kuwa karibu kuambulia pointi moja, lakini dakika ya 90+5, Jeancy Mboma aliifungia Singida bao hilo la ushindi na kuwaacha wenyeji na maumivu makali.
PAMBA Jiji imeendelea kujiweka katika nafasi ngumu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, baada ya leo kufungwa bao 1-0 dhidi ya Singida Black Stars, mechi iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Ikiwa nyumbani, Pamba Jiji ilionekana kuwa karibu kuambulia pointi moja, lakini dakika ya 90+5, Jeancy Mboma aliifungia Singida bao hilo la ushindi na kuwaacha wenyeji na maumivu makali.
Mboma hilo ni bao lake la pili Ligi Kuu Bara na ndiye aliyeibuka mchezaji bora wa mechi hiyo.
Pamba Jiji ilicheza muda mwingi ikiwa pungufu baada ya winga wake, Zabona Mayombya dakika ya 35 kuonyeshwa kadi nyekundu.
Kwa matokeo hayo, Pamba Jiji ipo nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi sita katika mechi kumi ilizocheza, imeshinda moja, sare tatu na kupoteza sita.
Singida imefikisha pointi 14 ikiwa nafasi ya sita, katika mechi tisa imeshinda nne, sare mbili, imefungwa tatu.
Pamoja na ushindani huo, Kocha wa Singida, Papy Kimoto, amesema haikuwa mechi rahisi, lakini wachezaji hawakukata tamaa dakika zote walizokuwepo uwanjani, hivyo juhudi zao zilizaa matunda.
"Mechi ilikuwa ngumu, ndiyo maana ushindani umepatikana dakika za mwisho, lakini kikubwa tumepata alama tatu zinazoendelea kutuweka nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi," amesema.
Kwa upande wa kocha wa Pamba Jiji, Francis Baraza, amesema: "Ingawa wachezaji wamecheza pungufu baada ya mwenzao kupata kadi nyekundu, nimeridhika na kiwango walichokionyesha, walipambana kwa kadri walivyoweza."