Yanga yawakumbusha mashabiki enzi za Bongo Fleva
Muktasari:
- Miongoni mwa wasanii waliopamba tamasha hilo ni Mwasiti, Chid Benz, T.I.D, Madee, Chege, Q Chilla na Mr Blue ambao kila mmoja alitumia muda wake jukwaani kutoa burudani na kuwafanya mashabiki kuimba na kucheza.
YANGA imeongeza ladha ya burudani katika tamasha lake kwa kuwakutanisha mastaa mbalimbali wa muziki Tanzania, huku majina yaliyowahi kutamba katika muziki wa Bongo Fleva yakipewa nafasi ya kupanda jukwaani na kuwaburudisha mashabiki.
Miongoni mwa wasanii waliopamba tamasha hilo ni Mwasiti, Chid Benz, T.I.D, Madee, Chege, Q Chilla na Mr Blue ambao kila mmoja alitumia muda wake jukwaani kutoa burudani na kuwafanya mashabiki kuimba na kucheza.
Ujio wa T.I.D ulikuwa sehemu iliyovuta hisia, kutokana na historia yake kubwa katika muziki wa Bongo Fleva. Msanii huyo ni miongoni mwa majina yaliyowahi kutawala anga la muziki Tanzania na bado ana uwezo wa kuwakumbusha mashabiki nyimbo na enzi zilizopita.
Kitendo cha Yanga, kuingiza burudani ya wasanii katika tamasha lake ni sehemu ya kulifanya tukio hilo kuwa zaidi ya shughuli ya soka.
Mashabiki wanapata si nafasi tu ya kushuhudia mastaa wapya wa kikosi hicho, bali pia burudani kutoka kwa baadhi ya wasanii wakongwe na wa kizazi cha sasa katika muziki wa Tanzania.
Burudani hiyo imelifanya tamasha hilo la Yanga Day linalofanyika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kuwa tukio linalounganisha soka, muziki na mashabiki.