Prime
Dakika 360 za moto Simba
MSHALE wa saa unaendelea kusogea kuelekea kwenye kipindi kigumu kwa Simba chini ya kocha Msauzi, Steve Barker ambaye sasa anakabiliwa na dakika 360 zitakazotoa picha muhimu ya mwelekeo wa kikosi hicho katika msimu wa 2026-2027.
Baada ya kuanza msimu kwa kushinda mechi tano mfululizo za Ligi Kuu Bara, Simba sasa inaingia kwenye kipindi ambacho kitahitaji zaidi ya ubora wa kikosi. Itahitaji uimara wa mwili, mbinu, usimamizi wa wachezaji na uwezo wa kocha kufanya uamuzi sahihi wakati presha inapoongezeka.
Mfululizo huo wa dakika 360 sawa na mechi nne, unaanzia Malawi, Septemba 6, Simba itakapokutana na Mighty Wanderers katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kabla ya kurejea Tanzania kwa ajili ya marudiano, Septemba 13 kisha siku tatu baadae, Septemba 16 watacheza dhidi ya Azam.
Baada ya hapo, Simba itaingia kwenye kipindi cha maandalizi kuelekea Kariakoo Dabi dhidi ya Yanga itakayopigwa Oktoba 10, huku mapumziko ya kalenda ya FIFA ya Septemba 21 hadi Oktoba 6 yakitoa nafasi kwa Barker kurekebisha maeneo yatakayohitaji maboresho.
Kwa Barker, hizi si dakika 360 za kawaida. Ni dakika ambazo zinaweza kuonyesha kama mwanzo mzuri wa Simba utageuka kuwa msingi wa msimu wenye mafanikio au kama changamoto za ratiba zitafichua mapungufu ya kikosi.
MWANZO WA KUVUTIA
Simba imeingia kwenye msimu huu kwa kasi kubwa, ikiwa haijapoteza pointi katika mechi zake tano za mwanzo za Ligi Kuu Bara.
Wekundu hao wa Msimbazi wameanza kampeni kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar, Pamba Jiji (2-1), Singida Black Stars (2-1), Coastal Union (1-0) na Geita Gold (2-0).
Ushindi huo umeifanya Simba kuanza msimu ikiwa na mwendo wa asilimia 100 huku Barker akianza kujenga taswira ya timu yenye uwezo wa kupata matokeo mazuri hata katika mazingira magumu.
Katika mechi tatu kati ya hizo, kikosi chake kililazimika kumaliza kikiwa pungufu kufuatia kuonyeshwa kadi nyekundu, lakini bado kikapata ushindi.
Huo ni mwanzo unaovutia, lakini changamoto kubwa sasa ni kama Simba inaweza kuendeleza mwenendo huo wakati inapokutana na wapinzani wenye ubora tofauti na huku ratiba ya kimataifa ikiingia katikati ya kampeni yake ya ligi.
DAKIKA 90 MALAWI
Dakika 90 za kwanza katika safari hiyo ya moto zitachezwa Septemba 6 nchini Malawi, ambapo Simba itakutana na Mighty Wanderers katika mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Huu ni mchezo ambao utahitaji umakini mkubwa kutokana na umuhimu wake katika hesabu za Simba za kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Barker anajua wazi kuwa matokeo ya mchezo wa kwanza yanaweza kuwa na athari kubwa kwenye mchezo wa marudiano, hivyo kikosi chake kitatakiwa kucheza kwa nidhamu na kuhakikisha kinapata matokeo yatakayoweka mazingira mazuri kabla ya kurudi Dar es Salaam.
Ushindi au sare yenye mabao inaweza kuipa Simba nafasi nzuri ya kumaliza kazi katika mchezo wa marudiano, wakati matokeo mabaya yanaweza kuongeza presha kwenye mchezo wa pili.
Mighty Wanderers ni miongoni mwa klabu zenye historia kubwa nchini Malawi, ikiwa imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara saba. Klabu hiyo ilianzishwa mwaka 1962 jijini Blantyre na ina historia iliyohusishwa na jamii ya Wareno waliokuwa nchini humo.
Historia yake pia ina uhusiano na FC Porto huku rangi ya bluu na nyeupe ikiwa sehemu ya utambulisho wa Wanderers.
Kwa sasa, Wanderers ipo kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Malawi ikiwa nafasi ya pili na pointi 29 sawa na vinara Silver Strikers, jambo linaloonyesha wazi kuwa Simba haitakutana na mpinzani mwepesi.
KABLA YA AZAM
Baada ya mchezo wa kwanza Malawi, Simba itarejea Tanzania ikiwa na jukumu la kujiandaa kwa mchezo wa marudiano dhidi ya Wanderers utakaochezwa Septemba 13. Hapo ndipo dakika 180 za mfululizo huu zitakapokuwa zimekamilika.
Mchezo huo unaweza kuwa na uzito mkubwa zaidi kwa sababu utatoa jibu la kwanza kuhusu kama Simba itaendelea na safari yake ya Ligi ya Mabingwa Afrika au italazimika kuangalia mashindano mengine.
Kwa Barker, hii itakuwa nafasi ya kuonyesha uwezo wake wa kusimamia mechi mbili za kimataifa ndani ya muda mfupi huku akihakikisha kikosi hakipotezi nguvu kuelekea majukumu ya ligi.
AZAM YASOGEZWA MBELE
Awali mchezo wa Simba na Azam FC ulipangwa kuchezwa Septemba 9, lakini sasa umesogezwa hadi Septemba 16, siku tatu baada ya kurudiana na Wanderers.
Mabadiliko hayo yanaipa Simba muda zaidi wa kupumua baada ya mechi za kimataifa, lakini wakati huohuo yanaifanya Septemba 16 kuwa siku nyingine muhimu katika safari ya Barker.
Azam ni timu ambayo Simba inapaswa kuiheshimu kutokana na ushindani uliopo kati ya klabu hizo katika miaka ya karibuni.
Msimu uliopita, Simba ilidondosha pointi dhidi ya Azam katika mchezo wa kwanza baada ya kutoka suluhu, kabla ya kupata ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa pili. Hivyo, Septemba 16 haitakuwa mechi ya kawaida kwa Simba. Itakuwa mtihani mwingine wa uwezo wa timu hiyo kuhamisha ubora wake wa kimataifa kwenda kwenye ushindani wa Ligi Kuu Bara.
Kwa upande mwingine, kuhamishwa kwa mchezo huo kunaweza kumpa Barker nafasi kubwa zaidi ya kupanga kikosi chake bila kulazimika kuwapeleka wachezaji kwenye mechi ngumu za ligi mara moja baada ya safari za kimataifa.
FUNGA KAZI
Baada ya kuzipangua dakika 270 za mwanzo, Simba itakuwa imesalia na dakika 90 ambazo zinaweza kuwa na uzito mkubwa zaidi katika mfululizo huo.
Ni dakika 90 za Kariakoo Dabi dhidi ya Yanga, Oktoba 10. Mchezo huo utachezwa baada ya siku 24 tangu kumalizika Mzizima Dabi kati ya Simba na Azam. Hivyo, tofauti na mechi tatu za kwanza, Barker atakuwa na angalau muda wa kujiandaa na mchezo huo licha ya uwepo wa kalenda ya FIFA lakini presha yake haitapungua.
Kariakoo Dabi ni mchezo ambao mara nyingi huwa na utofauti mkubwa, ni mchezo wa heshima, historia, ushindani na matarajio makubwa ya mashabiki.
Simba pia itakuwa na kumbukumbu ya msimu uliopita, ambapo ilishindwa kupata ushindi katika mechi zote mbili za ligi dhidi ya Yanga.
Mchezo wa kwanza uliochezwa Zanzibar ulimalizika kwa suluhu kabla ya timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa pili uliochezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam. Kwa hiyo, Oktoba 10, Barker atakuwa na kazi ya kuhakikisha Simba haipotezi tena pointi katika dabi hiyo.
MSIKIE BARKER
Baada ya kuiongoza Simba kuanza Ligi Kuu Bara kwa ushindi wa mechi tano mfululizo, Barker amekiri kuwa mwanzo huo ni mzuri, lakini anajua wazi kuwa changamoto kubwa bado iko mbele yao.
Kocha huyo amesema maandalizi ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika tayari yameanza, akisisitiza umuhimu wa kupata matokeo mazuri katika mchezo wa kwanza dhidi ya Wanderers.
“Kwa sasa tumeanza maandalizi ya mechi ya Ligi ya Mabingwa. Tunahitaji kuwa na mwanzo mzuri, kufanya vizuri katika mechi ya kwanza hata kama ni ugenini. Hilo litatupunguzia presha kwenye mechi ya marudiano, baada ya hapo sasa tutaendelea kuupa uzito mchezo mmoja baada ya mwingine,” alisema Barker.