Yanga yaitisha vikao vizito usiku
Muktasari:
- Kikao cha kwanza ambacho kitaanza muda mchache ujao kitakuwa ni kile cha Kamati ya Utendaji, ambacho ndio kinaonekana kubeba ajenda nzito.
Saa chache baada ya Yanga kulazimishwa suluhu dhidi ya TRA United, ndani ya klabu hiyo kuna vikao viwili vizito vinafanyika usiku huu.
Kikao cha kwanza ambacho kitaanza muda mchache ujao kitakuwa ni kile cha Kamati ya Utendaji, ambacho ndio kinaonekana kubeba ajenda nzito.
Kikao hicho kilichoitishwa na rais wa klabu hiyo injinia Hersi Said ambaye alikuwa uwanjani kwenye mchezo wa leo sambamba na Makamu wake Arafat Haji kimeitishwa kwa hali ya dharura.
Ingawa ajenda za kikao hicho imekuwa siri lakini Mwanaspoti linafahamu kwamba kati ya mambo yatakayojadiliwa ni pamoja na mwenendo wa timu hiyo.
Mbali na hilo Yanga itajadili maamuzi ya kulifuta benchi la ufundi la timu hiyo baada ya kuonekana mambo yanazidi kuwa magumu kwa kikosi hicho kwenye ligi.
Yanga mpaka sasa imeshaangusha pointi tano baada ya kufungwa na Simba 2-1 kisha sare ya leo mechi zote zikiwa za ugenini, ikisalia nafasi ya pili na pointi 18 baada ya kucheza mechi nane.
Kikao cha pili ambacho kutafuta ni kile cha wachezaji wa timu nzima ambacho litafanyika mara baada ya kikao cha kamati ya utendaji ambacho kinafanyika kwa njia ya mtandao.
Ndani ya kikao hicho cha wachezaji huenda ikatangazwa maamuzi hayo magumu ambayo yatatokana na kikao cha kamati ya utendaji.