Yanga vitani Ligi Kuu Bara
Muktasari:
- Baada ya kutoka kupata ushindi kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United kwa mabao 3-2, Yanga itaingia kwenye mechi hiyo ikiwa na hesabu mbili, ya kwanza ni kuendeleza kasi yake ya ushindi lakini pili kuwashusha presha mashabiki wake baada ya kuonekana kama ilikaribiwa kuzidiwa na Wabotswana hao.
YANGA inarudi uwanjani leo ikigeukia Ligi Kuu Bara, baada ya kutoka kucheza mechi ya kimataifa na kituo kinachofuata ni dhidi ya Geita Gold iliyorejea msimu huu ambapo wachimba madini hao watakuwa na dakika 90 za kujaribu kuzuia kasi ya mabingwa hao watetezi.
Baada ya kutoka kupata ushindi kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United kwa mabao 3-2, Yanga itaingia kwenye mechi hiyo ikiwa na hesabu mbili, ya kwanza ni kuendeleza kasi yake ya ushindi lakini pili kuwashusha presha mashabiki wake baada ya kuonekana kama ilikaribiwa kuzidiwa na Wabotswana hao.
Yanga ina rekodi bora mbele ya Geita, timu hizo zikiwa na rekodi ya kukutana mara sita kwenye ligi na Yanga ikiwa mababe kwa kushinda mechi zote, huku ikifunga jumla ya mabao 11 mbele ya wachimba madini hao kabla ya kushuka daraja.
Wenyeji Yanga wanahitaji ushindi lakini pia mabao mengi ili kuendelea kusalia juu ya msimamo, ikijua kwamba Simba kesho itakuwa uwanjani kwenye mechi ngumu dhidi ya Azam ambapo kama ikishinda basi tofauti ya timu hizo itaendelea kuwa ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Yanga kwenye ligi imekuwa na moto mkubwa ambapo kwenye mechi zake tano zilizopita, hakuna mchezo ambao imeshinda chini ya mabao mawili ,huku ushindi mkubwa ni wa mabao matano.
Geita itatakiwa kuwa makini na safu ya ushambuliaji ya Yanga washambuliaji Peter Shalulile mwenye mabao matatu, Cheikh Toure na Seleman Mwalimu ambao wamekuwa wakiwa na moto wa kufunga huku safu ya kiungo ya mabingwa hao ikiwa kwenye moto mkali.
Kocha wa Yanga Manqoba Mngqithi, akizungumzia mchezo huo alikiri kwamba wametoka kwenye mechi yenye presha dhidi ya Gaborone, huku akisema watakwenda kuitafuta ushindi mwingine mzuri ili kuendelea na hesabu za kutimiza malengo yao.
“Hii ni mechi nyingine, tumetoka kucheza mchezo ambao ulikuwa na presha kubwa, Geita sio timu nyepesi, tumeona namna imekuwa na mwanzo mzuri, wana wachezaji wazuri wenye uzoefu, tumepata siku chache za kujiandaa lakini tupo tayari,” amesema Manqoba
Geita ilianza vizuri msimu huu ambao imerejea ligi kuu ikishinda mechi mbili, ikapoteza mbili na kutoa sare moja ikiwa na kikosi cha wachezaji vijana na wale wenye uzoefu.
Matokeo bora sana kwao ni pale ilipowadhalilisha Kagera Sugar ikiwa nyumbani kwa ushindi wa mabao 6-2, ambao mpaka sasa ndio timu ambayo ilitengeneza ushindi mkubwa kwenye ligi.
Yanga itatakiwa kuwa makini na Geita hasa kwa wachezaji wake wawili wa zamani wanaoongoza safu ya ushambuliaji ya wachimba madini hao Mzambia Obrey Chirwa anayeshika nafasi ya pili kwa ufungaji akiwa na mabao manne na Yusuf Mhilu anayerejea kutoka kwenye maumivu.
Kocha wa Geita, Zuber Katwila, akizingumzia mchezo huo alisaema baada ya maandalizi ya kutosha timu yake ipo tayari kwenda kukutana na Yanga ambayo imeonyesha mabadiliko makubwa ya ubora msimu huu.
“Unapokutana na Yanga kila kitu kinajulikana hii ni moja kati ya timu bora ina wachezaji wenye wasifu mzuri lakini, tumejiandaa kutumia makosa yao wana mazuri yao na wanaweza kufanya makosa, tunataka kuyatumia makosa yao kutafuta ushindi au sare,” amesema Katwila.