Yanga njia panda Abuya kurejea dimbani
Kiungo wa Yanga, Duke Abuya. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Abuya aliumia katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kufanyiwa faulo na winga wa Simba, Libase Gueye. Pamoja na kupatiwa matibabu, kiungo huyo alijaribu kuendelea kucheza kabla ya kushindwa kuendelea dakika ya 25, hali iliyolazimu benchi la ufundi la Yanga kumtoa na kumuingiza Fredy Ngoma.
Kiungo wa Yanga, Duke Abuya, anakabiliwa na majeraha ambayo yanafanya kuwe na uwezekano wa kuwa nje ya uwanja kwa muda usiojulikana baada ya kuthibitishwa kupata jeraha la nyama za paja katika mchezo dhidi ya Simba, uliomalizika kwa Yanga kupoteza kwa mabao 2-1.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, amesema daktari wa timu hiyo, Moses Etutu, amethibitisha kuwa kiungo huyo amepata jeraha hilo, ingawa ukubwa wake na muda atakaohitaji kupona bado haujawekwa wazi.
Amesema uchunguzi zaidi wa jeraha alilopata Abuya utafanyika leo kabla ya matokeo kutolewa.
Abuya aliumia katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kufanyiwa faulo na winga wa Simba, Libase Gueye. Pamoja na kupatiwa matibabu, kiungo huyo alijaribu kuendelea kucheza kabla ya kushindwa kuendelea dakika ya 25, hali iliyolazimu benchi la ufundi la Yanga kumtoa na kumuingiza Fredy Ngoma.
Jeraha hilo limekuja wakati ambao Yanga inahitaji matokeo mazuri ili kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi, baada ya ushindi wa Simba kuifanya timu hiyo kufikisha pointi 21 na kuiacha Yanga nafasi ya pili ikiwa na pointi 18.
Kwa mujibu wa viwango vya kawaida vya majeraha ya nyama za paja, muda wa mchezaji kukaa nje ya uwanja hutegemea kiwango cha uharibifu wa misuli.
Daktari wa tiba za wanamichezo, Nassoro Matuzya, amesema kuna madaraja matatu ya majeraha ya nyama za paja kwa mchezaji.
Matuzya amesema jeraha la daraja la kwanza, ambalo huhusisha kuvutika kwa misuli au michubuko midogo, linaweza kumuweka mchezaji nje kwa siku saba hadi 21. Katika hali hiyo, mchezaji hupata maumivu kiasi na kwa kawaida huhitaji muda mfupi wa matibabu kabla ya kurejea mazoezini.
Amesema daraja la pili huhusisha kuchanika kwa baadhi ya nyuzi za misuli na linaweza kumuweka mchezaji nje kwa wiki tatu hadi nane. Jeraha la aina hiyo linaweza kuathiri uwezo wa kukimbia kwa kasi, kubadili mwelekeo na kupiga mashuti.
Matuzya amesema jeraha la daraja la tatu ndilo kubwa zaidi, likihusisha kuchanika kwa kiwango kikubwa au kukatika kabisa kwa misuli.
Amesema mchezaji akiumia kwa kiwango hicho anaweza kukaa nje kwa miezi miwili, sita au zaidi, kutegemea hali ya jeraha na matibabu anayopatiwa.