Prime
Yanga ilivyomkosa Girumugisha
WAKATI Yanga ikiimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao wa 2025-2026, imebainika kuwa mabingwa hao wa Tanzania walikuwa miongoni mwa klabu zilizokuwa kwenye vita ya kuwania saini ya winga wa kimataifa wa Burundi kutoka Al Hilal Omdurman, Jean Claude Girumugisha ambaye ametua Al Ahli Tripoli ya Libya kwa ada ya Dola 5.5 milioni (Sh14.5 bilioni).
Uhamisho huo umekuwa gumzo hapa jijini Kigali nchini Rwanda ambapo Al Hilal imepiga kambi, kutokana na ukubwa wa fedha zilizotumika huku ukiiweka timu hiyo ya Sudan katika nafasi nzuri kifedha baada ya kumuuza mmoja wa nyota wake muhimu.
Meneja wa Girumugisha, Patrick Gakumba, amefichua kuwa kabla ya Al Ahli Tripoli kufanikisha usajili huo, Yanga ilikuwa tayari imewasiliana naye ikitaka kujua uwezekano wa kumpata mchezaji huyo.
“Yanga ya Tanzania walinifuata kuhitaji saini ya mteja wangu Girumugisha, niliwaeleza kwamba kama wataweka mezani dola 1.5 milioni (Sh3.9 bilioni) hapo ilikuwa kabla ya timu nyingine kuwasilisha ofa yake, wakaniambia watarudi, lakini hawakurudi,” amesema Gakumba.
Jina la Girumugisha, lilikuwa likitajwa ndani ya Yanga, lakini dau hilo la kumng’oa pale Al Hilal likaonekana kuwa kubwa zaidi. Hata hivyo, Al Ahli Tripoli ilipoenda kumuhitaji, ikatajiwa kiasi kubwa zaidi ya kile ilichotakiwa Yanga, Walibya hao wakatoa na kumchukua.
Katika mechi 21 alizoichezea Al Hilal msimu uliopita 2025-2026 kwenye mashindano yote, Girumugisha alihusika moja kwa moja kwenye mabao 21, akifunga 11 na kutoa pasi 10 za mabao.
Takwimu hizo zilimfanya kuwa mmoja wa mawinga wenye mchango mkubwa zaidi katika soka la ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Kiwango hicho ndicho kilichozivutia klabu kadhaa, lakini Al Ahli Tripoli ndiyo iliyokuwa tayari kuvunja benki na kuwasilisha ofa kubwa zaidi, jambo lililoifanya Al Hilal kukubali kumuachia nyota huyo wa Burundi. Girumugisha anajiunga na Al Ahli Tripoli yenye mastaa wengine ambao wametua kipindi hiki cha usajili akiwemo mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele, Fagrie Lakay, Lamine Mamadou Camara na beki wa Algeria, Mohamed Amine Tougai.