Yanga, Azam ya sura mpya

ASILIMIA kubwa ya sura za mechi ya leo ya Yanga na Azam ni mpya tofauti na msimu uliopita.
Yanga na Azam mara ya mwisho walikutana Aprili 25 mwaka huu na Yanga kukubali kipigo cha bao 1-0 hadi sasa ni miezi sita tu lakini ukitaka kujua hiyo miezi ni mingi angalia vikosi vilivyoanza kwenye mchezo huo kwa timu zote kwani kwa asilimia kubwa wametimka na wengine hawana namba vikosini.
Kikosi cha Yanga kilichoanza kwenye mchezo huo ni Farouk Shikalo sasa hayupo baada ya mkataba wake kumalizika na kutimkia KMC. Mabeki walianza Kibwana Shomari bado yupo na ana uhakika wa kuanza leo.
Wengine ni Adeyum Saleh pamoja na kuendelea kubaki kikosini hana namba kutokana na Nabi kumuamini zaidi Shomari ambaye amemuhamisha namba, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ hana namba mbele ya Bakari Mwamnyeto.
Mwingine ni Dickson Job ameendelea kuwa bora na kuaminiwa na Nabi ni miongoni mwa nyota ambao walikuwepo kwenye mchezo uliopita, kiungo kiliundwa na Mukoko Tonombe ambaye ndiye alikuwa kiungo wa kutumainiwa ndani ya Yanga msimu ulioisha lakini sasa anahaha kurudi kikosi cha kwanza baada ya ujio wa Khalid Aucho na Yanick Bangala.
Nyota wengine walioanza kwenye mchezo huo na watakosa ujao ni Deus Kaseke ambaye nafasi yake ni kama imeporwa na winga Jesus Moloko, Michael Sarpong, Carlos Carlinhos wote wamevunja mikataba yao.
Wakati Yacouba Songne anaweza kuwa mchezaji wa tatu kati ya 11 waliocheza mchezo wa kwanza kuweza kucheza leo wakati Said Ntibanzokiza akikosa nafasi ya kucheza kutokana na kocha kumuamini zaidi Fei Toto ambaye mechi iliyopita alianzia benchi.
Kikosi cha Azam FC pia kina mabadiliko golini alianza Mathias Kigonya ambaye anatarajia kuanza leo. Mabeki walianza Daniel Amoah (anaweza kuanza na leo). Nico Wadada, Paskali Mshindo wote wamepoteza namba kikosi cha kwanza na sasa wapo Edward Charles na Lusajo Mwaikenda.
Mkongwe Aggrey Morris hatakuwa miongoni mwa nyota watakaoanza akiungana na Mudathir Yahya na Salum Abubakari kutokana na kusimamishwa kikosini kwa muda usiojulikana, Prince Dube ambaye alikuwa majeruhi amerudi na kuanza mazoezi hivyo ni uamuzi wa kocha kuamua kumpanga au kuto kumpanga.
Mchezaji mwenye uhakika wa kuanza kwenye mchezo huo ni Idd Seleman ‘Nado’ kutokana na ubora wake ndani ya timu hiyo wakati Ayub Lyanga pia amekuwa akisugua benchi kwenye michezo ya hivi karibuni hii ni kutokana na ujio wa Idris Mbombo.
Mkurugenzi wa ufundi wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Oscar Milambo alisema; “Mbinu za waalimu ndio zitatoa matokeo leo.”
Naye kocha wa Mwadui FC, Mohammed ‘Adolf’ Rishard alisema; “Yanga pamoja na kuwa na nyota wengi wapya tayari wameshapata muunganiko tofauti na Azam ambao bado wanajenga kikosi cha kwanza.”