Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yaliyomo kwenye nembo ya AFCON 2027

Muktasari:

  • Nembo hiyo iliyobuniwa kwa kuzingatia taswira ya ngao, imezinduliwa leo saa 7:00 mchana, ikiwa zimesalia siku 212 kabla ya mashindano hayo kuanza Juni 19, 2027.

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF), kwa kushirikiana na wenyeji wa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, Tanzania, Kenya na Uganda, limezindua rasmi nembo ya mashindano hayo, hatua inayozindua shamrashamra za kuelekea michuano hiyo mikubwa barani Afrika.

Nembo hiyo iliyobuniwa kwa kuzingatia taswira ya ngao, imezinduliwa leo saa 7:00 mchana, ikiwa zimesalia siku 212 kabla ya mashindano hayo kuanza Juni 19, 2027.

Uzinduzi huo ni sehemu ya maandalizi ya AFCON 2027, itakayofanyika kwa ushirikiano wa nchi hizo tatu za Afrika Mashariki chini ya jina la TotalEnergies CAF AFCON PAMOJA 2027.

Ubunifu wa nembo hiyo umebebwa na kaulimbiu isemayo: “Kuheshimu historia yetu, kusherehekea utamaduni wetu na kuashiria Afrika ya kesho”, inayolenga kuonyesha utambulisho na urithi wa mataifa mwenyeji.

NGAO INA MAANA GANI?

Kwa mujibu wa CAF, matumizi ya ngao katika nembo hiyo si ya bahati mbaya, bali yamechaguliwa kuwakilisha utambulisho wa Afrika Mashariki, ulinzi, fahari, udugu na umoja.

Ngao ni alama inayopatikana pia katika nembo za taifa za Tanzania, Kenya na Uganda, hivyo kuifanya kuwa kiwakilishi cha urithi unaozikutanisha nchi hizo.

Umbo la nembo hiyo limeundwa kwa duara mbili zinazokatana kwa usawa, huku likipambwa kwa nakshi za ushanga na michoro inayochochewa na sanaa za asili za ukanda wa Afrika Mashariki.

Katikati yake kuna taswira ya Kombe la AFCON, lililozungukwa na umbo la ramani ya Afrika, likiwa na ujumbe wa kuonyesha namna mashindano hayo yanavyounganisha ndoto, tamaduni na mataifa ya bara hilo.


RANGI ZA MATAIFA MATATU

Katika kuonyesha ushirikiano wa wenyeji wote, nembo hiyo imebeba rangi zinazotambulisha bendera za Tanzania, Kenya na Uganda.

Rangi nyekundu na nyeusi zimewekwa sehemu ya juu, huku kijani na njano zikitumika pembeni mwa taswira ya kombe na rangi ya bluu ikipamba sehemu ya chini.

Mbali na nembo kuu, CAF imezindua pia michoro 12 ya ngao inayotambulisha mataifa hayo matatu kwa kutumia alama na mitindo tofauti ya ubunifu.

Tanzania imetambulishwa kwa mistari ya mshazari inayotokana na muundo wa bendera yake, ikiwakilisha ardhi na utajiri wa maji.

Kenya imetumia mistari mipana ya mlalo kuonyesha nguvu na urithi wa taifa hilo, huku Uganda ikitumia rangi za joto na taswira ya ndege wake wa taifa, Korongo mwenye Taji.

Michoro hiyo itatumika katika mapambo ya viwanja vitakavyotumika kwenye mashindano hayo, mabango na majukwaa mbalimbali ya kidijitali duniani kote.

Jina PAMOJA limechaguliwa kuonyesha umoja na mshikamano wa Tanzania, Kenya na Uganda, huku likitumia Kiswahili kama lugha inayowaunganisha wananchi wa mataifa hayo katika safari ya kihistoria ya kuandaa AFCON kwa pamoja.

Mashindano hayo yatakuwa ya kwanza ya AFCON kuandaliwa kwa ushirikiano wa mataifa matatu ya Afrika Mashariki.