Wikiendi ya ‘Dabi’ Ligi ya Championship
Muktasari:
- Katika mechi za jana, Bigman FC iliyoishtusha Kigamboni United kwa kuichapa ugenini mabao 2-1, ilikuwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kucheza dhidi ya Bandari Tanzania iliyotoka kulazimishwa suluhu ya (0-0) na maafande wa Rhino Rangers.
LIGI ya Championship imeingia raundi ya 11, jana Ijumaa kwa mechi tatu kupigwa na nyingine tatu zikiendelea leo Jumamosi na mbili zikihitimishwa kesho Jumapili, huku kukiwa na dabi za kuvutia zitazochezwa wikiendi hii kwenye viwanja tofauti.
Katika mechi za jana, Bigman FC iliyoishtusha Kigamboni United kwa kuichapa ugenini mabao 2-1, ilikuwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kucheza dhidi ya Bandari Tanzania iliyotoka kulazimishwa suluhu ya (0-0) na maafande wa Rhino Rangers.
Kigamboni United iliyochapwa mabao 2-1, dhidi ya Bigman FC ya Tanga, iliendelea kubakia kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini, Dar es Salaam kujiuliza tena mbele ya maafande wa Rhino Rangers ya Tabora, iliyotoka suluhu (0-0) na Bandari Tanzania.
Mechi ya mwisho kwa jana Ijumaa, ilipigwa kwenye Uwanja wa CCM Kambarage, mkoani Shinyanga ambapo Stand United ‘Chama la Wana’ iliyochapwa na Mbuni FC mabao 2-0, iliikaribisha Transit Camp iliyotoka kuichapa Tabora United ya Tabora bao 1-0.
Leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Halmashauri ya Chunya jijini, Mbeya, itachezwa mechi ya kuvutia ya ‘Dabi ya Mbeya’, kati ya wenyeji KenGold FC iliyotoka kuichapa TMA FC ya Iringa bao 1-0, dhidi ya majirani zao maafande wa Tanzania Prisons.
Prisons inaingia katika mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu nzuri pia baada ya kutoka kuichapa KMC FC ya Kinondoni, jijini, Dar es Salaam bao 1-0, ushindi ulioifanya kusogea nafasi ya pili na pointi 20, nyuma ya Mtibwa Sugar yenye pointi 21.
Kwa upande wa KenGold iliyoshuka daraja msimu wa 2024-2025, ushindi wa bao 1-0, ilioupata dhidi ya TMA FC ya Iringa wiki iliyopita, uliifanya kufikisha pointi 12, ikiwa nafasi ya 12, baada ya kushinda mechi tatu, sare tatu na kupoteza nne.
Prisons inaingia katika mechi hiyo ikimtegemea mshambuliaji nyota wa kikosi hicho, Oscar Paul aliyefunga mabao saba kati ya 15, huku KenGold FC ikiwategemea Ibrahim Mtonga mwenye manne na Ibrahim Joseph Kilali aliyeifungia matatu hadi sasa.
Maafande wa Prisons walishuka daraja msimu wa 2025-2026, kupitia Play-Off, baada ya kumaliza nafasi ya 13 na pointi 32, huku ikicheza na kikosi cha Mbeya City kilichomaliza kikiwa nafasi ya 14 na pointi 30 na kutolewa kwa jumla ya mabao 2-0.
Baada ya hapo, timu hiyo ikacheza Play-Off nyingine ya kujinasua na janga la kushuka daraja dhidi ya Polisi Tanzania iliyoitoa Mbeya Kwanza kwa jumla ya mabao 7-1, kisha safari ya Prisons ikaishia hapo kwa kuchapwa jumla ya mabao 4-1.
Kocha Mkuu wa KenGold, Hussein Rupia alisema mechi ya leo itakuwa ngumu kutokana na mwenendo wa wapinzani wao hadi sasa, japo watapambana kupata ushindi nyumbani, huku akiwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuwapatia sapoti.
“Tunahitaji sapoti zaidi ya mashabiki zetu ili kuongeza morali ya wachezaji kupambana uwanjani, hii ni mechi kubwa na yenye ushindani kwa sababu timu zote zinatoka jiji moja, ila malengo yetu ni kubakia na pointi tatu,” alisema Rupia.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Prisons, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’, alisema ushindi wa mechi iliyopita umeongeza motisha ya kikosi hicho, ingawa, amewataka wachezaji wa kikosi hicho kucheza kwa nidhamu nzuri ugenini ili kupata matokeo mazuri.
“Kila mechi kwetu tunaichukulia kwa uzito mkubwa bila kujali ni ya dabi, malengo yetu ni kuhakikisha hadi kufikia raundi ya 15, tunaendelea kubakia nafasi nne za juu na ili kufanikisha hilo ni lazima tucheze kwa tahadhari,” alisema Nsajigwa.
Kwenye Uwanja wa Manungu Complex, mjini, Morogoro, vinara wa Ligi hiyo, Mtibwa Sugar yenye pointi 21, ikiwa kileleni mwa msimamo, baada ya kuichapa Songea United mabao 3-1, itaikaribisha Gunners FC iliyoichapa pia IAA SC ya Arusha mabao 3-1.
Katika mechi 10, za Mtibwa Sugar, imeshinda sita, sare tatu na kupoteza moja, ikifunga mabao 13 na kuruhusu saba, huku Gunners FC kutoka jijini, Dodoma ikishinda tatu, sare tano na kupoteza mbili, ikishika nafasi ya saba na pointi zake 14.
Mechi ya mwisho leo Jumamosi, itachezwa kwenye Uwanja wa Samora, mjini, Iringa, ambapo TMA FC iliyotoka kuchapwa bao 1-0, dhidi ya KenGold FC ya Mbeya, itaikaribisha KMC FC yenye kumbukumbu pia ya kupoteza 1-0, mbele ya Tanzania Prisons.
TMA FC iliyohamishia makazi yake Iringa ikitokea jijini, Arusha, imekuwa na mwenendo mbaya tangu kuanza msimu huu, baada ya kushinda mechi moja kati ya 10, huku ikitoka sare mbili na kupoteza saba, ikiwa mkiani nafasi ya 16 na pointi mbili.
Kwa upande wa KMC iliyochapwa mechi ya kwanza wiki iliyopita na Tanzania Prisons bao 1-0, iko nafasi ya tatu na pointi 19, baada ya kushinda tano, sare nne na kupoteza moja, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 17 na kuruhusu saba.
Raundi ya 11, itahitimishwa kesho Jumapili kwa mechi mbili kuchezwa, ambapo Tabora United iliyochapwa bao 1-0, dhidi ya Transit Camp, itaikaribisha Songea United, yenye kumbukumbu mbaya pia baada ya kutoka kufungwa na Mtibwa Sugar mabao 3-1.
Tabora United inashika nafasi ya 14 na pointi saba, baada ya kushinda mechi mbili, sare moja na kupoteza saba hadi sasa, huku Songea United ikishika nafasi ya 15 na pointi sita, kufuatia kushinda moja tu, ikitoka sare tatu na kuchapwa sita.
Mechi ya mwisho kesho itakuwa ni ‘Dabi ya Arusha’, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Aga Khan, jijini, Arusha, ambapo Mbuni FC iliyoichapa Stand United mabao 2-0, itaikaribisha IAA SC, iliyotoka kuchapwa ugenini na Gunners FC ya Dodoma mabao 3-1.