Kengold, Tanzania Prisons wavimbiana
Muktasari:
- Timu hizo za mkoani Mbeya zinakutana ikiwa kila upande unajivunia ushindi wa mchezo uliiopita, ikiwa KenGold iliichapa TMA bao 1-0, sawa na ushindi wa Prisons dhidi ya KMC.
ACHA wachapane. Ndivyo unaweza kuelezea wakati KenGold na Tanzania Prisons zikishuka uwanjani kesho Jumamosi kuwania pointi tatu katika Ligi ya Championship, huku rekodi na historia zikishtua.
Timu hizo za mkoani Mbeya zinakutana ikiwa kila upande unajivunia ushindi wa mchezo uliiopita, ikiwa KenGold iliichapa TMA bao 1-0, sawa na ushindi wa Prisons dhidi ya KMC.
Hadi sasa Prisons iliyoshuka daraja msimu uliopita ipo nafasi ya pili kwa pointi 20, huku KenGold iliyoshuka misimu mitatu nyuma ikiwa nafasi ya 12 kwa pointi 12 baada ya timu zote kucheza michezo 10.
Katika historia na rekodi, ndugu wamekutana mara mbili katika Ligi Kuu ambapo Tanzania Prisons imeshinda zote na sasa mchezo wa kesho utakuwa wa vita mpya, ambapo Maafande wakitaka kuendeleza ubabe, huku wachimba dhahabu wakitaka kuvunja uteja.
Straika wa Tanzania Prisons Oscar Paul amesema kila mchezo kwao ni vita ya pointi tatu ili kuendelea kubaki nafasi nzuri kwenye msimamo wa Championship, akiwataka nyota wake kuendeleza nidhamu uwanjani.
“Tunajua si mchezo mwepesi kutokana na ubora wa wapinzani, tunafahamu umuhimu wa mechi hiyo na lazima vijana wangu waende kwa tahadhari na nidhamu ili tufikie malengo” amesema nyota huyo mwenye mabao saba.
Kwa upande wake kiungo mshambuliaji wa KenGold, Charles Masai amesema baada ya kutokuwa na matokeo mazuri wakifululiza mechi nyingi ugenini, kwa sasa hesabu zao ni kushinda nyumbani.
“Tumekuwa na mechi tano mfululizo ugenini, sasa tunarejea nyumbani na hesabu zetu ni kuona hatupoteza pointi yoyote ili tuweze kujiweka pazuri, tunawaheshimu wapinzani ila pointi tatu ndizo muhimu” amesema nyota huyo.