Adeyum atamani rekodi mpya Mbuni FC
BEKI wa kushoto wa Mbuni FC ya jijini, Arusha, Adeyum Saleh, amesema moja ya malengo yake msimu huu ni kuivunja rekodi ya msimu uliopita wa 2025-2026, ambao nyota huyo alifunga mabao matano katika Ligi ya Championship akiichezea Bigman FC.
Akizungumza na Mwanaspoti, nyota huyo aliyewika na timu mbalimbali za Yanga, Coastal Union, Stand United, Kagera Sugar na Dodoma Jiji, amesema licha ya kucheza nafasi ya beki ila anahitaji kufunga kama ilivyokuwa wakati akiwa na Bigman FC.
“Msimu uliopita nilikuwa huru zaidi kucheza eneo la ushambuliaji nikitokea pembeni, msimu huu bado sijapata hiyo nafasi kwa sababu ni timu mpya na ninahitaji kuzoeana na wachezaji wenzangu, naamini ni suala la muda kwangu,” amesema Adeyum.
Aidha, Adeyum amesema kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi hicho cha kwanza cha jijini, Arusha, ni jambo linalompa motisha zaidi ya kuendelea kupambana kikosini, licha ya ushindani pia uliopo wa nyota wenzake na Ligi husika.