Wanne Pamba Jiji wamshusha presha Baraza
Muktasari:
- Pamba Jiji imecheza mechi sita msimu huu bila kupata ushindi, ikiwa na sare moja na vipigo vitano, huku matokeo yake yakitoka sare dhidi ya Dodoma Jiji,ikipoteza dhidi ya Simba, Azam, JKT Tanzania na Tabora mfululizo, hivyo imekusanya pointi moja tu, imefunga mabao matatu na kuruhusu 12.
KOCHA wa Pamba Jiji, Francis Baraza amepata ahueni baada ya kurejea kwa wachezaji wanne waliokuwa nje ya kikosi na uwepo wao umeongeza nguvu na chaguo katika timu hiyo ambayo imekuwa ikipambana na changamoto ya upana wa kikosi.
Pamba Jiji imecheza mechi sita msimu huu bila kupata ushindi, ikiwa na sare moja na vipigo vitano, huku matokeo yake yakitoka sare dhidi ya Dodoma Jiji,ikipoteza dhidi ya Simba, Azam, JKT Tanzania na Tabora mfululizo, hivyo imekusanya pointi moja tu, imefunga mabao matatu na kuruhusu 12.
Wachezaji ambao wamerejea kutoka majeruhi ni mabeki Abdulrahim Seif Bausi, Abdallah Said Ali ‘Lanso’ na Abdoulaye Yonta Camara mshambuliaji na kiungo Idriss Diomande ambao kwa sasa wameanza tena mazoezi na wenzao baada ya kurejea katika programu ya timu.
Akizungumzia kurejea kwa wachezaji hao, Baraza amesema ni hatua inayopunguza presha iliyokuwepo kwenye kikosi chake kutokana na kuwa na idadi ndogo ya wachezaji waliokuwa tayari kuitumikia timu.
“Kurejea kwa Bausi, Lanso, Yonta na Diomande ni hatua ambayo itatusaidia kuishusha presha. Angalau sasa kikosi kimeongeza watu wapya na tunapata chaguo zaidi,” amesema Baraza na kuongeza; .
“Wameshaanza mazoezi na ninaamini kwenye breki hii ya mechi za kimataifa tutaitumia vizuri kuwaweka sawa.
“Kipindi hiki cha mapumziko hakitakuwa cha kusubiri tu ratiba ya ligi kurejea, bali ni nafasi ya kurekebisha maeneo ambayo yameonekana kuwa na changamoto na kuhakikisha wachezaji wanaorejea wanapata utimamu unaohitajika.”