Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanahabari waweke wazi wanashabikia timu gani

Muktasari:

Wawe ni waandishi wa magazeti, mitandao ya jamii au watangazaji wa redio na televisheni, wanahabari wamekuwa na mchango mkubwa kote duniani hasa kipindi hiki ambapo dunia ni kama kijiji kwa jinsi habari za kona moja zinavyofikia ncha nyingine kwa haraka.

BILA wanahabari ni wazi kwamba soka haingekuwa na umaarufu mkubwa wala kufuatiliwa kutoka kona zote duniani kama ilivyo sasa, kwani ni wao walio kati ya wachezaji kwa upande mmoja na hadhira upande wa pili.

Wawe ni waandishi wa magazeti, mitandao ya jamii au watangazaji wa redio na televisheni, wanahabari wamekuwa na mchango mkubwa kote duniani hasa kipindi hiki ambapo dunia ni kama kijiji kwa jinsi habari za kona moja zinavyofikia ncha nyingine kwa haraka.

Nitangulie kusema kwamba kufika haraka kwa habari mpya ni jambo moja, lakini kufika kwa usahihi zikiwa na ukweli wake ni jambo jingine kabisa na hili ni moja ya mambo yanayozingatiwa kwa kiasi kikubwa na vyombo vya habari hapa na pia Magharibi kwa jumla.

Pamekuwa na katabia ka kudharau wanahabari za michezo, wakitofautishwa na wale wa ‘hard news’ ambapo hata hapa England kuna ambao wamekuwa wakitaniwa eti ni wa ‘kitengo cha toy’ kwa madai wanahabari wake hawajihusishi na masuala magumu kama ya uchumi, sayansi na kadhalika.

Hata hivyo, ni soka ambayo imethibitisha kuvuta kiasi kikubwa zaidi cha fedha katika mishahara, posho na hata katika kile ambacho kwenye taaluma nyingine ungesema kuajiri, maana mchezaji anafikia kutoka klabu moja kwenda nyingine kwa Pauni 85 milioni; mishahara na posho ni kubwa hivyo kwamba hakuna sekta nyingine zinazolipa hivyo.

Nikiisha kuweka bayana hayo, niseme kuwa soka ina utajiri, nguvu na ushawishi mkubwa sasa, ambapo mamilioni ya watu wanafuatilia ligi kuu na mashindano mengine makubwa duniani kila mara, ligi ya hapa - English Premier League (EPL) ikiongoza kwa umaarufu na kufuatiwa na Bundesliga ya Ujerumani, La Liga ya Hispania, Serie A ya Italia, Ligue 1 Ufaransa, Eredivise Uholanzi, Ukraine na nyinginezo.

England tulikuwa na gazeti maarufu - Sporting Life in Britain, lakini mengine makubwa kwa Magharibi ni L’Equipe hapo Ufaransa, La Gazzetta dello Sport Italia, Marca kule Hispania huku Wamarekani wanaokuja juu kwa soka nao wakiwa na magazeti na majarida kama Sports Illustrated na Sporting News, lakini pia redio na televisheni Eurosport, Fox Sports 1, ESPN na The Sports Network (TSN).

Ligi kubwa zimeanza msimu mpya pande kadhaa za Ulaya na watu wanafuatilia kwa karibu kupitia vituo vya redio, televisheni, intaneti na mitandao ya jamii, na hasa suala la usajili limekuwa na mvuto mkubwa.

Wanahabari wa hapa hutumia weledi na maadili kutekeleza kazi yao kama inavyotakiwa na sheria na kanuni, lakini vyama vyao vya kitaaluma vinawapa uhuru, kwa hakika angalizo, juu ya umuhimu wa kuwa wawazi.

Uwazi ninaouzungumzia ni juu ya timu zipi wanashabikia, maana kusema ukweli ni vigumu mwanahabari kutokuwa na timu, kwani hata ‘wazee’ wa kawaida mitaani wana timu zao, achilia mbali zile za miji yao, hujipembua kwa huyu kuwa Liverpool, yule Manchester United, wengine Arsenal, Chelsea au Blackburn.

Ukweli huu huwapa uhuru wa hali ya juu, na huwasababishia wanapofanya kazi yao kuwa makini zaidi, kwani hadhira inajua huyu ni shabiki wa timu fulani. Hisia za timu husika, hata hivyo, huwekwa kando kabisa wanapokuwa kazini.

Wakiisha kujua wanahabari wao ni wanaunga mkono timu gani, wakuu wao huwapanga kuandikia juu ya timu husika kwenye usajili, mechi, mgogoro au jambo jingine lolote kubwa, na katika hali hiyo wanahabari hao hutimiza kazi kwa ufanisi mkubwa.

Binafsi sijapata kujificha timu yangu; kwa miaka mingi nimeweka bayana mie ni Arsenal na sikosi kununua jezi kila msimu. Nafahamu fika pia kwamba watangazaji wengine walio katika Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), kama Charles Hillary, Salim Kikeke na wengineo wana klabu zao wanazoshabikia, lakini si wanapokuwa kazini.

Nimekuwa mchambuzi wa soka mechi zinapochezwa na watu hawa huendesha kazi zao kwa kufuata maadili, lakini baadaye masikitiko yao kwa timu ‘zao’ kufungwa husomeka nyusoni mwao, bali kazini hubakia kama macho yanacheka na moyo unalia. Kazi kwanza, maadili kwanza, ushabiki kando.

Hata hivyo, nijuavyo mie ni kwamba wanahabari wengi wa Afrika Mashariki huficha ushabiki wao kabisa, wala umma haujui wanashabikia timu gani, matokeo yake huishia kuhisi tu kutokana na jinsi wanavyotangaza au kukandia timu fulani kwenye makala zao, wakiandika kuonyesha kabisa kulia kwa sababu timu ‘yao’ ipo hovyo, lakini hadharani wakiulizwa hudai hawana timu, wakidhani ndiyo maadili hayo au sheria.

Ni vigumu mtu wa michezo kutokuwa na timu, ndiyo maana hata kwenye vyombo vya michezo wamekuwapo watu ambao ama walianza kuwa viongozi kwenye klabu au baada ya kutoka kwenye mashirikisho wamekwenda kuongoza klabu katika nafasi tofauti. Ni vigumu kuuzuia moyo kupenda.

Hili la kupenda na kuweka wazi lipo hata kwenye vyombo vikubwa hapa vya Uingereza kama televisheni za BBC na ITV. Mmoja wa watangazaji na wachambuzi maarufu kwenye televisheni na redio, Adrian Chiles, kwa sasa ni Mtangazaji Mkuu wa ITV Michezo ambapo mwaka jana alirudi BBC baada ya kuwa nje kwa miaka mitatu na akawa kwenye BBC Radio 5 Live.

Huyu aliweka wazi kabisa mapema, wenyewe wanasema ku ‘declare interest’ kwamba timu yake ni West Bromwich Albion na huko hukata tiketi za msimu mzima kwa ajili ya mechi na pia hutangaza katika programu rasmi za klabu zilizohifadhiwa katika DVDs.

Magari mawili ya Chiles yana herufu ‘WBA’ kwenye kibao cha namba za usajili lakini kana kwamba hiyo haitoshi, juu ya mlango wa nyumba yake, kuna kioo kilichoandikwa West Bromwich Albion kwa rangi na nembo za klabu hiyo.

Chiles ndiye mwandishi wa kitabu ‘We Don’t Know What We’re Doing’ kilichochapishwa mwaka 2007 na humo anasimulia maelezo ya washabiki wa damu wa klabu hiyo aliokutana nao katika msimu wa 2005/06, ambao mwishowe timu yake ilishuka daraja kutoka EPL na kinaonesha mahaba yake kwa WBA ambao hujulikana pia kama ‘Baggies’.

Wapo waandishi wengine wengi ambao wametumia fursa katika maisha yao kusaka habari za timu, wachezaji na watawala wa soka, ambazo kwa kweli wahusika hawangependa ama zichapishwe au zirushwe hewani.

Laura Williamson wa gazeti la Daily Mail ni mchapa kazi wa aina hiyo, lakini nje ya kazi, ni shabiki wa kutupwa wa Grimsby Town FC, ambapo kwenye mechi huuchora uso wake rangi za timu hiyo, nyeupe na nyeusi na alikuwa Wembley mwaka 1998 timu hiyo ilipotwaa ubingwa wa Kombe la FA.

Uwazi na ukweli utasaidia kuijenga zaidi tasnia ya habari, kwa namna ya pekee katika kitengo muhimu cha michezo, hususan soka. Tujifunze na tuige yale tunayoona yanatufaa kwetu nyumbani, mengine tuwaachie.